Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wanamorogoro kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupima Afya zao na kupatiwa ushauri wa bure na madaktari kutoka taasisi mbalimbali wanaotoa huduma hiyo, ambapo zoezi hilo la upimaji afya linatolewa bila malipo na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wito huo umetolewa Agosti 27, 2024 na Mkuu huyo wa Mkoa wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo kimkoa yanafanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Morogoro kwa kutoa huduma za Afya kwa wananchi.
Mhe. Malima amesema katika kuadhimisha maazimisho hayo, Jeshi hilo linatoa huduma za Afya zikiwemo upimaji wa macho, saratani ya shingo ya kizani na matiti kwa wananwake, upimaji wa tezi dume na huduma mbalimbali za kiafya hivyo amewata wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwenda kupima afya zao na kila mmoja anapopata huduma akawe balozi kwa mwenzake ili watu wazidi kujitokeza kwa wingi kupima Afya zao.
"... Naomba nichukue fursa hii niwasihi sisi sote tuliokuwa hapa tutumie nafasi hii twende tukapime Afya zetu, na tukitoka hapa twende tukawe mabalozi kwa wenzetu.."
Aidha Kiongozi huyo amelishukuru Jeshi hilo kwa huduma wanayotoa ya upimaji wa Afya bila malipo kwa wananchi wa Morogoro na isiwe mwisho kutoa huduma hiyo ya Afya bali waendelee kuitoa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zilizopo mkoani humo.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kutoa matibabu hayo bila malipo kwa wananchi wa Morogoro pia kuliongoza jeshi hilo na kuendelea kuwa imara zaidi ambapo imepelekea kujulikana kitaifa na kimataifa.
Sanjari na hayo Mhe. Malima amewataka Wananchi hasa wakinamama wajenge utamaduni wa kupima afya zao mara hususan magonjwa ya saratani katika mlango wa kizazi na matiti kwa lengo la kupata tiba mapema ili kukabiliana na changamato ya magonjwa hayo katika jamii huku akiwataka akinababa kujengea mazoea ya kupima tezi dume ili kuwahi matibabu pindi wanapogundulika kuwa unaugonjwa huo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga na Mkuu wa Kikosi cha Jeshi Mazao Brigedia Jenerali Seif Athumani Hamisi amesema shughuli ya utoaji wa huduma za Afya kwa Mkoa wa Morogoro zimeanza Agosti 26, 2024 na zimelenga kutoa huduma za upimaji bure kwa wananchi ambapo zoezi hilo litadumu ndani ya siku 5, hivyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupima Afya huku akibainisha huduma inayotolewa ni kwa magonjwa kama macho, saratani ya shingo ya kizazi na matiti, tezi dume, presha, kisukari na mengine mengi.
Naye Bi. Agnes sepeku mkazi wa manispaa ya morogoro akiwa amepata mara baada ya kupata huduma amesema huduma zinazotolewa ni zuri na zinatolewa kwa haraka ambapo amewataka wanamorogoro kujitokeza kwenda upima afya zao kwani hakuna gharama yoyote.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.