Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kutekeleza vema miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo huku akitoa angalizo kwa wasimamizi wa miradi hiyo kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anakagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari Boma.
Mhe. Adam Malima ametoa pongezi hizo Juni 22 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG za mwaka 2021/2022 katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akielekeza jambo kupitia ramani ya eneo la ujenzi wa shule mpya ya Boma.
Mkuu huyo wa Mkoa wakati akikagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya kata ya Boma, amepongeza kupata wazo la kujenga shule hiyo ambayo itaondoa changamoto ya watoto kusoma mbali pamoja na kuwapunguzia wazazi mzigo wa nauli, hivyo akaagiza ujenzi huo kukamilika kwa haraka ili mwakani wanafunzi waweze kuanza masomo.
Muonekano wa jengo la ghorofa tatu la shule mpya ya sekondari ya Boma iliyopo kata ya Boma.
“...mradi huu unamaslahi mapana sana kwa watoto wa hapa na wazazi wao...ndiyo maana nimesema mradi huu mmeangangalia mbali sana...” amasema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Adam Malima wakati akiwa kwenye kituo cha afya cha kata ya Tungi amepongeza wasimamizi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi huo na kutoa angalizo la kukamilisha kwa wakati.
Hapa Mhe. Adam Malima akiwa na viongozi wa chama cha Mapinduzi - CCM, Wilaya, Madiwani na watendaji wa Halmashauri hiyo wakikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Tungi.
Haya ni baadhi ya majengo ya kituo cha afya Tungi hatua za umaliziaji unaendelea.
Katika hatua nyingine Mkuu akiongoza kikao cha Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri hiyo amewasisitiza Wahe. Madiwani kusimamia miradi ya maendeleo, na kuiagiza Menejimenti ya Halmashauri hiyo kuandaa taarifa za matumizi ya fedha zaidi ya shilingi bilioni 29 zilizokusanywa kuanzaia mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani.
Kwa upande wake Mkaguzi wa nje na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuendelea kupata hati safi kwa kipindi cha miaka sita mfululizo.
Mkaguzi wa nje na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga.
Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo ametembelea ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Boma ambayo itagharimu shilingi bilioni 1.1, ujenzi wa kituo cha Afya Tungi kitakachogharimu shilingi bilioni 1, ujenzi wa jengo la utawala shule ya sekondari Mkundi Mlimani pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji Kata ya Lukobe.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.