Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameipongeza timu ya Vijana chini ya miaka 20 ya Mtibwa Sugar ambayo imekuwa bingwa wa mashindano ya Vijana chini miaka 20 mara tano mfululizo, ikiwemo ubingwa wa mwaka huu, huku akiwataka viongozi wa timu hiyo kuweka mikakati madhubuti kuiendeleza timu hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwasalimia wachezaji wa timu ya Mtibwa Sugar ya vijana chini ya miaka 20 mara baada ya kuwasili Ofini hapo.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Julai 7 mwaka huu wakati wa hafla fupi ya kuipongeza timu hiyo kwa kuwa bingwa mara tano mfululizo ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa msimu huu wa 2022/2023.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambapo Mkuu wa Mkoa huo Adam Malima aliandaa chakula kwa ajiri ya kuwapongeza kwa ushindi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima (wa tano kushoto waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wachezaji, viongozi wa timu ya Mtibwa Sugar pamoja na Viongozi wa Serikali kwenye hafla ya kuipongeza timu hiyo.
Mkuu wa Mkoa amesema kufanya vizuri kwa timu hiyo mara tano mfululizo ni jambo zuri, Vijana hao wakitunzwa vizuri wataleta mafanikio hadi kwenye timu ya Taifa, ili kufanikisha hilo amewataka viongozi wake kuwaendeleza Vijana hao ikiwa ni pamoja na kuwapandisha kuchezea timu kubwa ya Mtibwa Ili kupata uzoefu.
"...sasa Mimi nakuombeni hawa wachezaji ambao wametuthibitishia kuithamini Mtibwa na nyinyi muwathamini..." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Adam Malima amekubali ombi la viongozi wa timu hiyo la kuwa mlezi wa Mtibwa Sugar, hivyo ameahidi kufuatilia suala la viwanja ambavyo walikuwa wameahidiwa ili kuongeza maeneo ya kuendeleza vipaji vya vijana Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na viongozi, wachezaji na wadau wa sekta ya michezo wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya Mtibwa Sugar.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameitakia mafanikio timu ya Wanawake ya Ifakara Queens ambayo inaenda kushiriki mashindano ya wanawake Mkoani Mwanza hivi karibuni.
Awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa timu hiyo Bw. Abel Magesa alimshukuru Mkuu wa Mkoa na kumpongeza kwa kuwa mdau wa michezo na kwamba wanaamini sekta ya michezo Mkoani hapa sasa itafanya vizuri.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa timu ya Mtibwa Sugar Bw. Abel Magesa akito shukrani kwa Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Bw. Abel amewasilisha ombi kwa Mkuu wa Mkoa la kuwa mlezi wa timu hiyo pamoja na kuwasaidia kupata viwanja walivyokuwa wameahidiwa na viongozi waliopita.
Nae, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu Mkoa wa Morogoro kwa niaba ya viongozi wa Chama hicho wameahidi kutoa ushirikiano kwa Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha kuwa sekta ya michezo Mkoani humo inazidi kukua.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akizungumza wakati wa hafla ya kuipongeza Mtibwa Sugar.
Kwa upande wake Athuman Makambo mfungaji bora wa mashindano hayo kwa mwaka huu amesema michezo ilikuwa migumu lakini kujituma kwao kuliweza kuwafanya kuwa mabingwa, hata hivyo, ameiomba Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) kuhakikisha kuwa mashindano yajayo yanaboreshwa.
Katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa ametoa zawadi ya jezi, mipira na fedha taslim Tsh. 1,000,000 ikiwa ni pongezi kwa timu hiyo kufanya vizuri.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Herman Tesha (kulia) akiwa pamoja na Mhe. Rebeca Nsemwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro wakati wa hafla ya kuipongeza Mtibwa Sugar.
Afisa Michezo Mkoa wa Morogoro Bi. Grace Njau (kushoto) akiwa na Afisa Elimu wa Mkoa huo Bi. Germana Mng'aho wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya Mtibwa Sugar.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.