Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amezishauri Taasisi za Wakala wa mbegu za Kilimo - ASA na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania – TARI Mkoani humo kuzalisha mbegu bora za michikichi ili kuwashawishi wananchi kujikita katika uzalishaji wa zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiangalia miche ya michikichi kwenye moja ya kitalu kilichopo kwenye shamba la msimba Wilayani Kilosa.
Mhe. Malima amesema hayo Juni 11 mwaka huu alipotembelea Taasisi za Wakala wa mbegu za Kilimo - ASA na Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania – TARI Wilayani Kilosa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG Mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ili kuwahamasisha wanamorogoro kulima zao hillo la michikichi inatakiwa mbegu bora hivyo watahamasika kulima zao hilo kwa tija.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akisaini kitabu cha wageni katika shule ya Msingi Mhovu mara baada ya kuwasili shuleni hapo kwa lengo la kukagua ujenzi wa shule hiyo.
“...kama tunataka watu wa morogoro wavutiwe na kilimo hiki cha michikichi, mbegu sahihi ni kila kitu...” amesema Mhe. Adam Malima.
Sambamba na hayo Mhe. Adam Malima amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri tano za Malinyi, Ulanga, Kilosa, Mlimba na Ifakara kuandaa maeneo kwa ajili ya vitalu vya michikichi ambayo itastawishwa na kuwagawia wananchi katika maeneo yao.
Hapa Mkuu wa Mkoa anakagua ujenzi wa shule shikizi ya Mhovu Wilayani Kilosa.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amewataka wafugaji kuheshim jamii wanayoishi nayo kwa kutoingiza mifugo yao katika mashamba jamii hizo na kama watakaidi agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa mbegu za Kilimo - ASA Dkt. Sophia Kashenge amesema ASA imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uzio wa Shamba la Msimba kwa gharama ya shilingi bilion 1.3, ukarabati wa gereji milioni 400, uzalishaji wa mbegu milion 300 na kufufua shamba la Msimba.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa mbegu za kilimo - ASA Dkt. Sophia Kashenge akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu shughuli wanazozifanya.
Sambamba na hilo Dkt. Sophia amesema katika shamba hilo wanalima mazao ya alizeti, mtama na choroko na kuahidi kuwa baada ya kukamilika kwa mifumo ya umwagiliaji watazalisha mazao mengi Zaidi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.