Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameitaka taasisi ya Sokoine University Graduate Entrepreneurs Coorparative (SUGECO) ya Mkoani humo kuhakikisha wanawatafutia hekari 200 wananchi wa kijiji cha Lubungo zitakazowasaidia kulima na kuzalisha mazao ya bustani ili kuinua kipato chao na Mkoa kwa ujumla.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Novemba 7, 2024 wakati akizindua mradi wa vijana wa kilimo cha mazao ya bustani kibiashara chini ya Programu ya Beyond Farming Collective (BFC) ambapo uzinduzi huo umefanyika katika kata ya Lubungo, Kijiji cha Lubongo Halmshauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Amesema, wananchi wa Kijiji cha Lubongo wametoa ardhi yao kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ili waweze kuwanufaisha hivyo ameitaka taasisi ya SUGECO kuhakikisha wanawasaidia wananchi hao kutenga hekari 200 ili waweze kugawana na kuzalisha mazao hayo ya hustani.
"... Lubungo wamekupeni shamba ili nyie na wao wanufaike nalo, kwa hiyo wao wamekupeni hekari 200 na wao wataweka ekari 200 pembeni na lazima mzitafute .." Amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Malima amewasisitiza wafugaji wa Mkoa wa Morogoro kufuga kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa na kuacha ule ufugaji wa mifugo mingi isiyo na tija kwa mfugaji, hivyo amewahimiza wafugaji kuvuna mivugo yao na kufuga kisasa zaidi.
Katika hatua nyingine ameipongeze taasisi ya SUGECO na wadau mbalimbali kwa kushirikiana pamoja kutekeleza mradi huo kwa vitendo huku akiwataka wadau wote kuendelea kutekeleza mradi huo ili kuyafikia malengo ya kukifanya Kijiji cha Lubungo kuwa cha mfano katika uzalishaji wa kisasa wa mazao ya bustani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUGECO Mr. Revocatus Kimario amesema mradi huo unagharimu zaidi ya shilishi Bilioni 1.13 ambapo unaenda kuwanufaisha vijana wasiopungua 1,820 huku akibainisha mazao yatakayozalishwa katika mashamba hayo kuwa ni matikiti maji, vitunguu na matango
Mr. Kimario ametoa wito kwa vijana wa Mkoa wa Morogoro hususan vijana wa kijiji cha Lubongo kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa miundombinu yote ya uzalishaji wa kisasa inaenda kukamilika hivyo ni wajibu wao kutumia mradi huo kuzalisha mazao ya bustan huku akiwahakikishia kuwepo kwa masoko ya uhakika wa mazao yatakayozalishwa.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka wananchi wa Kijiji cha Lubungo kuupokea mradi huo kwa mikono miwili ambapo amesema utawasaidia kulima kilimo chenye tija, pia ameitaka taasisi ya SUGECO kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kulima mazao yatakayowapa kipato.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.