Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kutoka Morogoro hadi Kilosa kwa lengo la kuangalia hatua ya ujenzi iliyofikiwa pamoja na usalama wa treni hiyo inayotarajia kuanza safari zake katikati ya mwezi Julai 25, mwaka huu
Mhe. Malima amefanya ziara hiyo Julai 4, 2024 akiambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka treni hiyo kuanza safari zake kwa kipande cha Morogoro – Dodoma ifikapo Julai 25, Mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ameridhishwa na utendaji kazi unaoendelea wa kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu ambayo ilikuwa haijakamilika ikiwemo ujenzi wa uzio (Fence) kwa ajili ya kuzuia wanyama pori kama tembo pamoja na mifugo huku akiagiza kazi hiyo ikamilike ifikapo tarehe 15 - 18 Julai.
“…sisi watu wa Morogoro tulipokea salamu, ya kwamba kuanzia tarehe 25 mwaka huu zitaanza safari za abiria kwenda Dodoma lakini kwa muda sasa, zaidi ya mwezi tuliweka angalizo kwa eneo hili…” amesema Mhe. Malima
Akikagua kituo cha treni cha Kilosa Mkuu huyo wa Mkoa amesema Kituo hicho cha treni cha Kilosa ni cha kimkakati kwa kuwa kitasaidia kukuza sekta ya Utalii Mkoani humo kwani amesema wageni wengi watakaotumia usafiri wa SGR wataweza kushuka Kilosa na kisha kutembelea Vivutio vilivyopo Mkoani humo vikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, Hifadhi ya Milima ya Udzungwa, na vivutio vingine vingi vilivyopo eneo hilo.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi wanaojihusisha na wizi wa miundombinu ya Reli hiyo zikiwemo Nyaya za shaba huku akiwaonya kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria na mpaka sasa amesema tayari kuna baadhi ya watu wameshatiwa mbaroni wakihusishwa na wizi wa vifaa vya mradi huo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Kituo cha treni cha mwendokasi cha Kilosa kitafungua milango ya kiuchumi hususan katika sekta ya Utalii, Kilimo na Mifugo ambapo kumewekwa mkakati wa kushawishi watalii kutoka ndani na nje ya nchi kuanza kutembelea Vivutio na uwekezaji uliomo ndani ya Kilosa kupitia Reli ya SGR.
Hata hivyo, Mhe. Kabudi amebainisha kuwa Wilaya ya Kilosa ina utajiri wa kilimo cha mazao mbalimbali likiwemo zao la Vitunguu na mpunga hivyo kutokana na urahisi wa usafirishaji wa mazao hayo kutachochea uzalishaji wenye tija na kujenga Uchumi wa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa jumla.
Naye, Mkurugenzi wa Miundombinu wa Shirika la reli Tanzania Mhandisi Machibya Shiwa amesema zoezi la kuweka uzio limefikia 95% huku maeneo ya ushoroba wa Ngerengere na ushoroba uliopo katikati ya Kimambila na kimamba ni maeneo yanayojengwa uzio maalum wa kudhibiti wanyama wakiwemo tembo wanaotoka mbuga ya Mikumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.