Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekasirishwa na tabia ya wananchi hasa wafugaji wa Mkoani humo wanaoingiza mifugo yao kwenye hifadhi na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Mhe Malima ametoa kauli hiyo Januari 18, 2024 wakati wa ziara yake na kutembelea pori la akiba la mto Kilombero lililopo Wilayani Kilombero ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi wa Mkoa huo.
Mhe. Malima amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) wanampango wa kutengeneza msitu wa hifadhi unaozunguka hifadhi nzima utakaokuwa na upana wa mita 200 ili kuzuia Wafugaji kutoingiza mifugo yao katika eneo la hifadhi hiyo.
“….Hakuna mtu anauchukia ufugaji, Tunataka ufugaji uwe endelevu ili uwe na manufaa kwa Tanzania kwa miaka 50 ijayo na wakulima wawepo, na ng’ombe ziwepo, hatuishi kwa ajili ya leo tu….” amesema RC Malima.
Pia Mhe. Adama Malima amesema, wana lengo la kuwawekea hereni ng’ombe wote watakaokuwepo eneo la bonde la Mto Kilombero ili kufahamu idadi yao katika eneo hilo, hivyo kuwa rahisi kujua wanapoongezeka na kuchukua hatua mapema.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa wafugaji wanaolisha mazao ya wananchi kwa makusudi watakaobainika watalipa hasara yote itakayotokea, na kwamba hataki kusikia migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa sababu pande hizo mbili zinategemeana, kwa wafugaji kupata malisho na wakulima kupata mbolea kutoka kwa wafugaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafugaji Kijiji cha Miwangani Parasoi Ndimba amesema wapo tayari kupunguza idadi ya mifugo na kupangiwa maeneo mengine kulingana na idadi ya mifugo wanayomiliki ili kupunguza ongezeko la mifugo katika eneo hilo.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amemuomba Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Malima kutatua changamoto ya maji wanayokumbana nayo hususan kipindi cha kiangazi hasa katika Kitongoji cha Miwangani ambapo tatizo hilo kwa sasa limekuwa sugu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.