Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kuendekeza tabia za majungu na migongano kazini kwa sababu zao binafsi na kusababisha kuzorota kwa shughuli za Serikali hususani ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Juni 24, 2024 wakati wa kikao cha Baraza maalum la wahe. Madiwani kwa ajili ya kupitia na kujadili hoja za Ukaguzi kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Ifakara.
Mhe. Malima amesema kuna baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Ifakara wanaendekeza majungu na migongano hata kwa kiongozi wao ambaye ni Mkurugenzi hivyo kushindwa kutekeleza vema majukumu yao na kusababisha Halmashauri hiyo kuzidi kuzama huku akiwanyooshea kidole wahe. madiwani kushindwa kusimamia hali hiyo.
" .. Hatuwezi tukakaa kimya huku Ifakara inazama wao wanamagomvi nyie madiwani mnamagomvi hamsimamii miradi haiwezekani.." amesisitiza Adam Malima.
Aidha Kiongozi huyo amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo na wahe. madiwani kujitathimini wao kama wapo kwa maslahi yao binafsi waache mara moja bali wafanye kazi kwa maslahi ya umma na kuwaletea wananchi maendeleo wanayohitaji.
" Kama wewe ni diwani nenda kajitathimini uko upande wa Diwani maendeleo au uko upande wa Diwani maslahi binafsi, kama wewe ni mtendaji kajitathimini, kama wewe ni mtendaji maendeleo au mtendaji maslahi binafsi..." amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Kassim Faya Nakapala ameonesha masikitiko yake ya kutokamilika kwa wakati ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri hiyo unaogharibu zaidi ya shilingi Bil. 7.4 ambapo ujenzi huo unatekelezwa na Tanzania Building Agency (TBA).
Akitoa salam kwenye kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali Mkoani humo Dkt. Mussa Ali Musa ametumia fursa hiyo kuwataka wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kupeleka Banki fedha zote za makusanyo katika Halmashauri zao kabla au ifikapo Juni 30. mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kesho Juni 25 , 2024 ataendelea kuongoza kikao cha baraza la Madiwani kama hicho cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika HalmShauri ya Wilayani ya Kilosa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.