Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea tabia ya baadhi ya Viongozi Mkoani humo kutokamilisha miradi ya Maendeleo kwa sababu ya uwepo wa maelewano mabovu baina yao, hivyo kuwacheleweshea Wananchi Maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya alipotembelea ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Lipangalala.
RC Malima ametoa kauli hiyo ya karipio Novemba 8 mwaka huu wakati wa ziara yake alipotembelea ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Lipangalala iliyopo katika Halmashauri ya Mji Ifakara Wilayani Kilombero Mkoani humo.
Akiongea na Viongozi wa Wilaya hiyo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara amesema, kuendeleza ugomvi ambao unasababisha ucheleweshaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo shule ya mpya ya Sekondari ya Lipangalala ni kuwacheleweshea wananchi maendeleo na hivyo akawataka kuacha tabia hiyo la sivyo atachukua hatua.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Lipangalala.
“...kabla ya Rais Samia hajafanya maamuzi mimi nitakuwa nimeshawasimamisha ili yeye akafanye maamuzi mengine huko juu...” amesema Mkuu wa Mkoa Adam Malima.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo kuchunguza chanzo cha ucheleweshaji wa ujenzi wa sekondari hiyo ambao ulitarajiwa kukamilika Oktoba 23, 2023 na kwa sasa bado upo katika hatua za kujenzi wa kuta.
Maagizo yake kwa vingozi hao kwa sasa ni kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi huo kuendelea kujenga usiku na mchana ikibidi na kwamba anataka ukamilike kabla au ifikapo Disemba 31 mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Ndg. Solomoni Kasaba amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wake wanapata huduma wakati wote huku akidai kuwa Chama hakitavumilia uzembe katika ukamilishaji wa miradi ya maendeleo kwa sababu ya mabishano ya viongozi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Lena Nkaya ameeleza sababu za ucheleweshwaji wa ujenzi wa shule hiyo kuwa ni pamoja na mchakato wa manunuzi kuchukua muda mrefu na upatikanaji wa mkandarasi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo mpya ya sekondari ya Lipangalala Msimamizi wa ujenzi huo Bw. David Chaula amesema mradi huo unagharimu shilingi milioni 528 ambapo inajumuisha ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa, jengo la utawala, chumba cha TEHAMA, Maktaba na vyumba 3 vya maabara.
Haya ni baadhi ya majengo katika shule mpya ya Sekondari ya Lipangalala inayoendelea na ujenzi.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 1 mwaka huu na ulitarajiwa kukamilika mwezi OKtoba 23,2023 ambapo Mkuu wa Mkoa ameagiza ukamilike ifikapo tarehe 31 Disemba, 2023.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.