Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea vikali ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa wajane kutokana na kuwepo kwa mila na desturi kandamizi katika jamii na kufanya maisha ya wajane kuwa magumu zaidi baada ya kufiwa na Waume zao.
Mhe. Malima ametoa karipio hilo Juni 23, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya Wajane duniani katika Viwanja vya Kiwanja cha ndege kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo yakiwa na lengo la kubaini changamoto za wajane na kutafutia ufumbuzi, kusimamia haki na kudumisha upendo baina yao.
"...semeni mtapata msaada wa haraka... na nina maafisa maendeleo kutoka ofisini kwangu ili mjue serikali ni moja na inahakikisha hamnyanyaswi na ujane..." amesema Mhe. Adam Malima
Aidha, Mhe. Adam amesisitiza Chama cha wanawake wajane Tanzania - CCWWT kuweka utaratibu wa kutegemea Sheria kwa kushirikiana na mahakama ili kuwa na mifumo wezeshi mfano Dawati la Jinsia katika kupinga ukatili kwa kina mama na kupata haki zao ukiwemo urithi wa mali.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amesema chama hicho kina jukumu la kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wajane Milioni 1.4 kutokana na sensa ya mwaka 2022 hapa nchini ili kujua namna ya kupata haki zao pasipo kutegemea vikao vya mila vinavyodidimiza maslahi ya kina mama wajane kwani Serikali inatambua na kuthamini uwepo wa wajane hao.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutambua umuhimu wa kina mama na kufanya jitihada kuja na mpango wa nishati safi kwa matumizi ya nyumbani kuepuka uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti ovyo na kuondoa magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni.
Kwa upande wake, Mratibu wa Wajane Taifa ( Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum) Bi. Bahati MaJwala amesema maadhimisho hayo yanasaidia kuongeza uelewa kwa Jamii kuhusu mila na desturi hivyo kuwajengea uwezo wajane kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro Bi. Mary Carlos Kallomo amesema mahakama imeboresha mifumo na kuhakikisha inawawezesha watu wote hapa nchini wakiwemo wznawake wajane kupata haki zao za msingi.
Kwa niaba ya Wanawake wajane, Katibu wa Chama cha Wajane Tanzania Bi. Sabrina Tenganamba amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 idadi ya wanawake wajane imefikia Milioni 1.8 hapa nchini huku akibainisha kuwa ndugu wa wajane hao hawaruhusiwi kuchukua mali zao bali hurithiwa na watoto pamoja na Mama zao.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.