Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema serikali ya Mkoa huo haitomvumilia mlanguzi yeyote anayenunua mazao kwa wakulima kienyeji na kwa bei ndogo kwani serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ina nia njema kuanzisha mfumo wa stakabadhi za ghala ili kuwanufaisha wakulima.
Mhe. Malima amesema hayo Mei 7, Mwaka huu wakati akifungua kikao cha tathmini ya mfumo wa stakabadhi za ghala kilichofanyika katika Halmashauri ya Ifakara Mji Wilayani Kilombero kikiwa na lengo la kubaini changamoto zilizojitokeza msimu wa 2024/2025 na maandalizi ya msimu mpya wa 2025/2026.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametaka kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, watumishi wa serikali pamoja na wanasiasa ili kuleta mapinduzi ya kilimo Mkoani Morogoro na kuwa mfano bora barani Afrika katika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Mhe. Adam Malima amesema wakulima wanapaswa kuuza mazao yao kupitia mfumo wa Stakabadhi za ghala kwani mfumo huo umeongeza bei za mazao likiwemo zao la kakao kutoka kilo 1 kuuzwa Tsh. 4,000 hadi Tsh. 28,000 hivyo kuinua uchumi kwa wakulima nataifa.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa huo unahitaji kuzalisha tani 20,000 za ufuta zitakazoingiza Tsh. Bil. 80 kutokana na mfumo wa Stakabadhi ghalani na kukuza vipato vya wakulima.
Mazao mengine ya biashara yanayolimwa Mkoani humo ambayo yanatakiwa yapitie mfumo huo wa stakabadhi za ghala ni pamoja na Mbaazi, Kakao, Korosho na karafuu ambapo huongeza mapato ya ndani kwa kiasi kikubwa Mkoani humo kupitia mfumo huo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji Mkoani Morogoro Bi. Beatrice Njawa amesema kutokana na changamoto zinazodaiwa kucheleweshwa kwa malipo ya stakabadhi ghalani Serikali ya Mkoa imetengeneza kamati ya kuhakikisha malipo ya mazao ya mfumo huo kulipia kwa wakati.
Naye, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro Bi. Cesilia Filimin amesema mfumo wa stakabadhi za Ghala umesaidia kuwepo kwa soko la uhakika kwa mazao yanayolimwa Mkoani humo huku akibainisha kuwa kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu mfumo huo kwa wakulima ni moja ya changamoto inayopelekea baadhi ya wakulima kuendelea kuuza mazao yao kwa walanguzi.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.