Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekerwa na migogoro ya ardhi inayoendelea katika Kijiji cha Kambala kilichopo katika Wilaya ya Mvomero ambapo amedai kuwa migogoro hiyo inazolotesha maendeleo kijijini hicho, Wilaya na Mkoa kwa jumla.
Mhe. Malima ameyasema hayo Januari 7 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kambala kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi Mkoani Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Kijiji hicho ambacho kilitakiwa kuwa mfano wa maendeleo kama maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona Tanzania inakuwa na maendeleo mazuri badala yake Kijiji hicho ‘kimegubikwa’ na migogoro ya umiliki wa ardhi inayopelekea umasikini kwa wakazi wake.
“...nimeletewa taarifa za migogoro, migongano na mitafaruku ya Kambala...imenikera sana...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, Mhe. Malima ameahidi kupeleka timu ya wataalam wa ardhi ikiongozwa na Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Morogoro Bw. Frank Minzikuntwe ili Kwenda kuweka michoro ya maeneo yenye migogoro na kumaliza migogoro hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewashauri wafugaji katika Kijiji hicho na Mkoa mzima kwa ujumla kufanya ufugaji wao kuwa wa kibiashara ili kuinua uchumi wao, Wilaya na Taifa kwa ujumla huku akibainisha kuwa matarajio yake ni kuona wafugaji hao wanakuwa mfano kwa wafugaji wengine hapa nchini.
Lakini pia amewatka wafugaji hao kuonesha umuhim wao kwa jamii inayowazunguka na Serikali kwa jumla kwa kuchangia miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya Maji, Afya na Elimu kwani kwa kufanya hivyo watajijengea heshima na kuthaminiwa.
Kwa upande wa wafugaji akiwemo Tesha Saning’o, wameeleze kuwa changamoto zinazowakabili kijijini hapo ni Pamoja na ukosefu wa maji kwa ajili ya mifugo na matumizi yao huku Mganga Mfahi wa zahanati ya Kambala Dkt. Daniel Saninga amesema Sekta ya Afya inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi na nyumba za watumishi ambapo amesema kwa sasa watumishi hao wanaishi katika baadhi ya vyumba vya zahanati hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.