Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwapa mahitaji muhimu wakati huu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Hayo yamesemwa Disemba 30, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima alipokuwa anatoa zawadi mbalimbali kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye vituo vya kulelea watoto vya Amani Center na Mission to the Homelesss Children vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Kwa sababu hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapenzi yake kwa Watoto hao wanaoishi katika makao ya kulelea Watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia zawadi za krismas na mwaka mpya 2025.
“… nimekuja hapa kwa maelekezo mahsusi ya Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan amenituma na kusema nenda ukawafikie watoto vituoni kwa kadri utakavyojaaliwa nimefika lakini nitakaa na Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kuona tuwafikie watoto wengi zaidi…” Amesema Mhe. Adam Malima
Aidha, Mhe. Adama Malima amesema ofisi yake itatoa ushirikiano wowote kwa lengo la kufanikisha kuwasaidia watoto hao kupata huduma muhimu zikiwemo huduma za afya, elimu na huduma nyingine muhimu zitakazowawezesha kuwajengea uwezo makundi hayo maalumu na kupata fursa za kushiriki kazi mbalimbali katika jamii ili kujikwamua na umaskini.
Awali, akiwa katika kituo cha Amani Centre Mhe. Adamu Malima alimuagiaza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Emmanuel Mkongo kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa kina ndani ya wiki moja suala la Bima ya Afya kwa watoto wote 181 wa kituo hicho ili wapate Bima hiyo ya Afya.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa akiwa kituo cha Mission to the homeless Children kilichopo kata ya Kihonda ameagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwenda kuangalia barabara inayokwenda kituoni hapo na kuifanyia matengenezo maeneo yote korofi ili kuondoa usumbufu wanaoupata watoto wanapokwenda shuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mission to the Homeless children Bw. Robert Lameck ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kutekelaeza lengo lao la kukuza watoto hao ambapo amesema hadi sasa kituo kimewezesha kulea watoto ambao wengine wamefanikiwa kwenda kupata Elimu ya Chuo Kikuu zikiwemo shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu huku wengine kupata kazi mbalimbali zikiwemo Ualimu wa shule za msingi na sekondari, ufisa ustawi, tarafa na kata, utafiti, afisa magereza na kilimo
Msaada huo wa Mhe. Samia Suluhu Hassan wenye thamani ya shilingi Milioni mbili na laki mbili katika vituo vyote viwili umejumuisha mchele kilogram 200, unga wa ugali kilogram 200, unga wa ngano kilogram 100, sukari kilogram 100, mafuta ya kupikia lita 40, mbuzi wawili, viungo, vinywaji, mafuta ya kupaka na sabuni.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.