Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima amemwomba Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaongezea muda Madaktari Bingwa aliowaleta Mkoani Morogoro kutoa matibabu kwa wananchi (Outreach Services) ambapo wananchi wengi wameonekana wana uhitaji wa kuonana na Madaktari hao, hivyo amemwomba Dkt. Samia kuwaongezea muda ili kukidhi kiu ya wananchi wake.
Mhe. Malima ametoa ombi hilo Mei 7, Mwaka huu wakati akizindua rasmi Kambi ya huduma za matibabu za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Kanda ya kati zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuanzia Mei 6 na 10, 2024.
"...tumwombe Mama Samia, nyie si mnatumia jina lake Madaktari wa Mama Samia kwa hiyo tumuombe ili awaelekeze mpige nyingine kama hii maana bado kuna Watanzania wengi sana ambao wamechelewa kupata taarifa hizi na wanatamani sana kuja kupata huduma yenu..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kuwawezesha madaktari Bingwa 55 kupitia Wizara ya Afya kushiriki katika kambi hiyo aliyoiita ni kambi kubwa kuliko kambi zote alizowahi kuziona kwa kipindi chote alichofanya kazi Serikalini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Hospitali kutoka Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian Mayengo amesema Wizara ya Afya itaendelea kuratibu mazoezi kama hayo kwa sababu ya mwitikio wa wananchi ni mkubwa hali inayoonesha kuna uhitaji huo wa wananchi kupata matibabu.
Aidha, amebainisha kuwa hadi kufikia Mei 7, 2024 tayari idadi ya watu zaidi ya 7000 kwa nchi nzima wamefikiwa na zoezi hilo la kupata matibabu kupitia kambi mbali mbali hapa nchini zinazoendelea kutoa huduma kama hiyo kupitia Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba hadi kufikia siku ya Ijumaa ya Mei 10, 2024 watu wengi watakuwa wanufaika wa kambi hizo.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Pwani (Tumbi) Dkt. Aman Malima ambaye pia ndiye Mwenyekiti waKambi hiyo ya Kanda ya Kati amesema, Kambi hiyo inayojumuisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida, Pwani na Morogoro hadi jana Mei 7, 2024 imekwisha hudumia wagonjwa zaidi ya 1500 ambapo wagonjwa 33 wamefanyiwa upasuaji wa macho, koo na magonjwa ya mifupa, na kubainisha kuwa kwz mwitikio huo, zaidi ya wananchi 3000 wanatarajiwa kuhudumiwa kambini hapo.
Katika kuhakikisha serikali inasogeza huduma za Afya karibu na wananchi, Wizara ya Afya kushirikiana na hospitali za Rufaa za Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Singida na Pwani (Tumbi) wizara itaendelea kuratibu zoezi hilo ili kutoa huduma hiyo ya Afya kwa wananchi kupitia kambi maalum zilizoelezwa hapo juu.
Magonjwa yanayopewa kipaumbele kutibiwa katika kambi hiyo ni pamoja na magonjwa ya watoto, wanawake na uzazi, masikio, pua na koo, upumuaji, magonjwa ya ndani (Moyo, figo, kisukari na shinikizo la damu), mfumo wa mkojo, mifupa, ngozi, macho, kinywa na meno, Afya ya akili, utengamao, mfumo wa chakula na huduma ya usingizi tiba na ganzi.
Awali kambi hiyo ya Kanda ya Kati ya Huduma za matibabu za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipangwa kufanyika kuanzia Mei 6 hadi 10 , 2024 huku wananchi wote wenye uhitaji wa tiba kutoka mikoa mitano ya Pwani, Iringa, Dodoma, Singida na Morogoro wanahamasishwa kufika katka kambi hiyo au kupiga simu 0683435656 au 0783658931.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.