RC Malima aongelea Utajiri wa Morogoro, asema Uchumi wake uko katika sekta ya Kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Uchumi wa Mkoa huo unapatikana katika sekta ya Kilimo kwa kuwa Mkoa huo una ardhi yenye rutuba, maji ya kutosha na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha mazao karibu yote muhimu yanayolimwa hapa nchini.
Mhe. Malima amesema hayo Machi 26, 2024 wakati wa kongamano la Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na kilimo (TCCIA) lililofanyika hoteli ya Nashera, Manispaa ya Morogoro likishirikisha watu mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na taasisi za Kibenki.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Malima amesema, ili Wakazi wa Morogoro waweze kukuza Uchumi wao, wanawajibika kuanza kulima kisasa kwa kuwa kwa sasa suala sio kulima pekee, bali kulima kulingana na uhitaji wa soko.
“……. Lazima tufanye kilimo cha uzalishaji chenye tija kinachoendana na uhitaji wa Soko la nchi zingine hususan Nchi ya India…” Amesema Adam Malima.
Akizungumzia mahusiano baina ya Tanzania na India, mbele ya mwakilishi wa Balozi wa India Bw. Manoj Verma Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha umuhim wa Mkoa wa Morogoro kwenye mahusiano hayo kuwa yanatokana na utajiri wa Mkoa huo kwenye Sekta ya kilimo.
Amesema, kupitia mahusiano hayo, Mkoa wa Morogoro utanufaika kupitia Kilimo, kwa sababu India iko mbali kiteknolojia hivyo Tanzania wakiwemo wakazi wa Morogoro watapata ujuzi wa kilimo chenye tija kutoka India hususan kuzalisha mazao yao kwa wingi na kuboresha mazao hayo kulingana na masoko ya kimataifa.
Mhe. Malima amesema, mwaka 2024 Mkoa umejipanga kuzalisha miche milioni moja ya zao la mikarafuu na miche hiyo inatarajiwa kupandwa katika safu za milima ambayo imeharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata mkaa, kuni pamoja na kilimo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Mwadhine Mnyanza amesema lengo la kongamano hilo ni kuboresha mahusiano baina ya Nchi ya India na Serikali ya Tanzania hususan Mkoa wa Morogoro na Sekta binafsi ili kujenga uelewa wa Pamoja na kuweka mikakati inayotekelezeka husuan katika sekta ya kilimo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Morobatiki Group Dkt. Herriet James amesema kongamano hilo litaongeza uhusiano na litasaidia kupata malighafi ikiwemo upatikanaji wa rangi kwa bei nafuu na kwa urahisi hivyo litaongeza uzalishaji wa bidhaa ya Batiki.
+++++++++++++++ ++++++++++++
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.