RC MALIMA ARIDHIKA NA UJENZI WA DARAJA LA RUAHA, AMSHUKURU RAIS, WADAU NA WANAHABARI
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam kighoma Malima ameridhika na maendeleo ya ujenzi wa daraja la mto Ruaha baada ya kufika eneo la ujenzi na kukuta kazi zinaendelea kufanyika huku ikiwa imebaki asilimia 9 tu ujenzi wa Daraja hilo kukamilika.
Hayo yamebainika Mei Mosi, 2024 wakati Mhe. Kighoma malima alipofanya ziara ya siku moja kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake ulisimama kutokana na Mvua zilizokuwa zinanyesha.
Mhe. Malima amesema, ujenzi wa daraja hilo kwa sasa unaendelea vizuri baada ya hali ya mvua kusimama na ujenzi kuendelea na kupelekea watu kuvuka kwa miguu kutoka upande mmoja hadi mwingine na kuleta matumaini ya kukamilika kwa Daraja hilo.
“….lakini namshaukuru mwenyezi mungu (at least - angalau) hapa tulipo Daraja kutoka upande mmoja hadi upande mwingine limeezekwa kama sote tulivojionea…” Amesema Mhe. Malima
Katika hatua nyingine, Mhe. Kighoma Malima ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa maelekezo Mawaziri na Watendaji wengine kufika Mkoani Morogoro na kujionea hali halisi ya mafuriko na kutoa Ushauri na misaada mbalimbali, ombi lake kubwa na kuiomba Serikali kufungua mawasiliano kwa maeneo ambayo bado hayajafunguka.
“…tunachotaka sisi ni kufunguliwa tu mawasiliano…” amesema Adam Malima
Aidha, amewashukuru wadau wote waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kutoa misaada ya hali na mali kwa wananchi wa Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga waliofikwa na mafuriko yaliyotokana na mvua nyingi zilizonyesha kipindi kifupi kilichopita.
Mwisho, lakini si kwa umuhimu, amewashukuru waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro kwa kutoa taarifa sahihi kuonesha uhalisia wa mafuriko yaliyotokea ndani ya Mkoa wa Morogoro hususani wilaya za Kilombero, Mlimba na Ulanga na kupelekea viongozi wa kitaifa kufika na kujionea hali ya mafuriko hayo.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa ujenzi wa Daraja hilo akiongelea ujenzi wa Daraja la Ruaha amesema ujenzi huo umefikia asilimia 91, na ujenzi wa mradi wote wa Barabara ya Kidatu - Ifakara kwa jumla umefikia asilimia 89 huku akibainisha kuwa daraja hilo litakamilika katikati ya mwezi Juni, mwaka huu endapo mvua hazita endelea kunyesha.
Wananchi wa Wilaya ya Kilosa na Kilombero wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga Daraja hilo kubwa kwani wamesema awali kulikuwa na changamoto ya watu kugombania kupita kwa vile lilikuwa jembamba, lakini pia Daraja la zamani lilikuwa lina vyuma juu kiasi kwamba kama kuna gari ina mizigo mikubwa ililazimu kupunguza kwanza kabla ya kupita.
Hata hivyo wamesema kwa sasa wanafurahi kwa ujio wa Daraja hilo kwa kuwa ni pana linatoa nafasi ya kupishana magari kwa magari bila bughudha huku watu wakiwa wamewekewa njia yao pembeni mwa Daraja hilo lakini pia Daraja hilo litasaidia kuvusha mazao yao kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.