Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema ameridhishwa na ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro baada ya kukamilisha sehemu ya ujenzi wa majengo hitajika na kutoa baadhi ya huduma ya Afya kwa wananchi wake.
Mhe. Malima ameyasema hayo Juni 20, 2023 wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyopo takriban km 100 kutoka Mjini Morogoro.
Amesema, uwekezaji wa hospitali hiyo uliofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unalenga kusaidia wakazi wa Halmashauri hiyo hivyo kupunguza umbali wa zaidi ya 100 km Kutoka Mvuha kwenda Morogoro mjini ambako walikuwa wanakwenda kupata matibabu.
"...ni mafanikio makubwa sana na kama hapa tulipo mimi mwenyewe nimefarijika sana, namshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu Kwa kuwekeza kwenye mambo kama haya..." Amesema Mhe. Adam Malima.
Sambamba na Hilo, Mhe. Malima amesema ingawa hospitali hiyo haijakamilika kwa asilimia mia lakini imeendelea kutoa huduma ili kunusuru uhai wa Watanzania wa Halmashauri hiyo huku akiagiza kuweka kipaumbele katika kukamilisha majengo na utoaji wa huduma kwa akina mama, watoto na huduma ya maabara.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza watendaji wanaosimamia ujenzi huo kuongeza Kasi ya utekelezaji Kwani amesema uwiano uliopo wa majengo manne yanayotoa huduma kati ya majengo 14 hauridhishi.
Sambamba na agizo hilo amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuongeza idadi ya watumishi katika Hospitali hiyo zaidi ya 22 kuja kusaidiana na wengine 32 waliopo ili kupunguza majukumu kwa watumishi waliopo na kuleta tija kwa wagonjwa.
Awali, Mkuu huyo wa Mkoa akiwa katika kituo cha afya cha Mikese ameagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (RUWASA) kuchimbwa visima virefu vya maji ya uhakika ili kuondoa adha ya uhaba wa maji katika kituoni hicho cha Afya na kusaidia wananchi wa maeneo jirani.
Katika hatua nyingine akiwa katika kijiji cha Tambuu, Mhe. Adam Malima ameahidi kutoa miche ya zao la michikichi 5,000 ambayo wataigawa kwa wakazi wa Kijiji hicho kilichopo kata ya Lundi na kwamba kila kaya itapewa miche mitano ya kupanda kwenye mashamba yao lengo ni kuwaongezea wananchi zao hilo la biashara ili kuongeza kipato chao na kuongeza pato la Taifa
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Morogoro Dkt. Kazimili Emanuel Subi, amesema hospital hiyo inawasaidia wakazi wa eneo hilo kutotembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya huku akibainisha uwepo wa madaktari bingwa watakao kuwa wanaletwa mara kwa mara hospitarini hapo ili kusogeza huduma za upasuaji karibu zaidi na wananchi.
Miongoni mwa wagonjwa akiwemo Bi. Fatuma Kibwana amewashukuru madaktari kwa kazi nzuri wanayoifanya na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea hospitari hiyo kubwa na yenye tija kwao.
Hospitali hiyo ya wilaya imeanza kutoa huduma za Afya tangu mwaka 2021 kukiwa na wastani wa wagonjwa 5 kwa siku na sasa inapata wagonjwa zaidi ya 30 kwa siku ikitoa huduma ya wagonjwa ya kulaza wagonjwa, maabara, mionzi, x-ray pamoja na ultrasound.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.