Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Taasisi hizo hususan katika ujenzi wa Madaraja na Barabara huku akitoa maagizo kwa watendaji wa Serikali kutoa Elimu kwa wananchi wa Berega na vijiji jirani kutunza miundombinu hiyo ambayo ndio chachu ya kukuza uchumi na kuisaidia kupata huduma muhimu za Afya, Elimu Maji na usafirishaji.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 4 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo.
Mhe. Malima akiambatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa amefanya ziara hiyo katika wilaya za Kilosa na Mvomero kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ya barabara.
Miundombinu aliyotembelea kiongozi huyo ni pamoja na ufukuaji mchanga katika Daraja la Dumila, Karavati zinazojengwa barabara ya Morogoro - Dodoma eneo la Mvomero na ujenzi wa daraja la Berega.
Miradi mingine ni ujenzi wa karavati yanayojengwa barabara ya Kilosa - Mikumi na Daraja la Luhemba ambako liko Wilayani Kilosa.
Akiwa Katika mradi wa daraja la Berega ambako ujenzi wake utagharimu shilingi Bil. 7.9 hadi kukamilika kwake, amewaagiza watendaji wa Wilaya hiyo akiwemo Afisa Tarafa, Mtendaji Kata na watendaji wa Vijiji kuhakikisha wananchi wa Berega na maeneo jirani wanatunza miundombinu ya daraja hilo kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa baina ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga, lakini pia litasaidia wananchi kufika kwenda Hospitali ya Berega kupata matibabu kipindi chote cha mwaka tofauti na awali ambapo kulikuwa na changamoto hususan kipindi cha masika.
Aidha, amewataka wananchi hao kutofanya shughuli za kijamii kando Kando ya mto wa daraja hilo hususan shughuli za kilimo ili daraja hilo liweze kudumu kwa muda mrefu.
"...nimefarijika sana na mradi huu katika hatua iliyofikia, kwa hakika tuna kila sababu ya kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kupata Daraja kubwa namna hii...hivyo nawaomba sana wananchi wa vijiji jirani kuacha kulima maeneo yaliyokaribu na miundombinu kama huu kwa ajili ya kulitunza lizidi kubaki imara..." amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema daraja hilo lina manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa watanzania wote kwa ujumla hivyo hakuna budi kulilinda.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa akiwa katika Mradi wa ujenzi wa Daraja la Ruhembe Wilayani Kilosa amesema Serikali imetoa fedha kutekeleza miundombinu kwani inategemewa na watanzania katika shughuli za kiuchumi na kijamii na kuwataka Wakandarasi wa mradi huo kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kukamilisha Daraja hilo kwa matumizi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema Daraja la Berega litakapokamilika litasaidia kwa sehemu kubwa kwenye usafilishaji wa bidhaa ikiwemo za nafaka kwa kipindi chote cha mwaka hivyo uchumi wa Kilosa utakuwa maradufu.
Nae, Mhandisi Maghesa Khamis , Mkandarasi mzawa katika Mradi wa Daraja la Berega akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo amesema mradi umefikia 99% ambapo utakamilika Oktoba 8, mwaka huu na Daraja hilo kuanza kutumika rasmi.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.