Siku chache baada ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kutoa agizo la kutoa pole na misaada ya mahitaji muhimu kwa waathirika wa Halmashauri ya Mlimba kupitia usafiri wa anga (Helicopter ) kutokana na miundombinu ya Halmashauri hiyo ikiwemo Barabara kuharibiwa na kusababisha kutokufikika katika maeneo ya kata ya Masagati na Utengule limeanza kutekelezeka.
Agizo hilo limeanza kutekelezwa aprili 26, 2024 ambapo likisimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya maafa Mkoani humo ikiwa usafiri huo unatokea Ifakara Mji kupeleka misaada Halmashauri ya Mlimba Wilayani Kilombero.
"... na mkumbuke Waziri Mkuu alisema nini alisema hapa kuna orodha ya wahanga sasa ndio wanaokusudiwa kwanza jamani kuna watu wamepoteza kila kitu kwanzia nyumba, chakula na shamba hao ndio wapewe kipaumbele..." amesema Malima
Aidha, Mhe. Malima amesema mahitaji hayo ni zaidi ya tani 6 ambayo yametoka serikali kuu na kwa wadau mbalimbali wakiwemo wa sekta binafsi na sekta za umma na kuungwa mkono na Wabunge wa Wilaya hiyo katika kufanikisha wananchi wanasaidiwa kulingana na uhitaji wakiwa na lengo la kutoa pole na kuwafariji waathirika wa janga la mafuriko Wilayani humo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa mahitaji ya Mkoa ni mengi kulingana na mafuriko yanayoharibu miradi ya maendeleo na makazi ya wananchi pamoja na mazao yaliyo mashambani, hivyo wananchi wa Wilaya za Malinyi na Ulanga serikali inaendelea na mchakato wa kuwafikia ili kutoa msaada.
Kwa upande wake, Kamishina msaidizi mwandamizi wa Jeshi la zimamoto na uokoaji ambaye ni mratibu wa maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Ivan Alfred Ombela amesema kuwa mchakato huo wa upelekaji wa misaada ya chakula mbalimbali ikiwemo mchele, maharage, sukari, na unga katika Halmashauri ya Mlimba ambapo kuna jumla ya waathirika 1900 kwenye kata mbili za Masagati na Utengule.
Pia, ameongeza kuwa katika kata hizo Kamati za maafa za kata zinahakikisha waathirika wote wa mafuriko kupata mahitaji hayo kutokana na utaratibu uliopangwa.
Naye, Bi. Rainoda Peter Kilangavana Mkazi wa Masagati ameishukuru serikali kwa kutoa misaada mbalimbali katika kata hiyo na kuiomba serikali sikivu kutatua changamoto ya Kituo cha Afya baada miundombinu kuharibiwa hivyo kina Mama wajawazito kushindwa kupata huduma kwenda Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Mlimba.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.