Mkuu wa Mkoa wa Morgoro Mhe.Adam Kighoma Malima amesema wajumbe wa baraza la ushauri la chuo huria kituo cha Morogoro wanataka kukiendeleza Kituo hicho kuwa cha mfano hapa nchini kwa kukiendeleza na masomo katika ngazi za shahada, stashahada, na astashahada za fani mbalimbali.
Mhe. Malima amesema hayo Februari 10 mwaka huu alipotembelea na kufanya kikao cha baraza la ushauri katika chuo hicho cha Huria kituo cha Morogoro kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, ameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zitasaidia ujenzi wa maabara pamoja na madarasa ya ziada yatakayosaidia kubeba wanafunzi wengi na kuondoa changamoto wakati wanachuo wanafanya mitiani.
“….. Sisi kama baraza la ushauri lazima tujikite kwa ajili ya kukifanya hiki kituo chetu cha Morogoro kiwe ni kituo cha mfano kwa vituo vyote vya Tanzania nzima…” amesema Adam Malima.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amefarijika kuona idadi kubwa ya wanafunzi wakijiandikisha katika chuo kikuu hicho huria kituo cha Morogoro wakiwemo walimu wa shule ya msingi.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amejitolea kugharamia usajili wa walimu 30 wanaojisajiri katika chuo hicho kwa kuwalipia shilingi 200,000 kila mmoja kwa walimu wale wa kwanza watakao jiandikisha katika ngazi ya astashahada ya uwalimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Machela amewataka Watumishi wa Serikali hasa kada ya ualimu kuchangamkia fusa hiyo ili kuweza kujiendeleza hali itakayosaidia walimu hao kuongeza maarifa katika utendaji wao wa kazi.
Naye Mhadhiri wa chuo kikuu Tanzania kituo cha Morogoro Dkt. Wambuka Rangi amesema chuo hicho kinakumbana na changamoto ya technolojia, ambapo wanashindwa kuwapata wananfunzi wanapo fundisha kwa njia ya mtandao (video conference) kwa sababu baadhi ya yao wanatoka maeneo yenye kunachangamoto ya mtandao (internet).
Dkt. Rangi ameongeza kuwa chuo hicho kinatoa elimu za aina tofauti tofauti kwa ngazi mbalimbali zikiwa za muda mfupi na za muda mrefu lengo likiwa ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa kila mtu na kwa kila kundi kulingana na uhitaji wake.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.