Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemtaka msimamizi wa ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuongeza kasi ya ujenzi huo ambao hadi sasa umefikia asilimia 50.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Novemba 21 mwaka huu wakati akikagua ujenzi wa Ofisi hiyo mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuangalia maendeleo ya ujenzi huo na hatua iliyofikia.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa ujenzi huo unatarajia kukamilika ifikapo May 2024 ambapo hadi sasa imebaki miezi 6 hadi mradi huo kukamilika hivyo amemtaka msimamizi wa ujenzi huo kuongeza kasi ya ujenzi ikiwezekana ukamilike kabla ya wakati.
“...jengo zuri kama hili la Mkuu wa Mkoa limekaa mahari pazuri, mandhari nzuri, umeme upo, mchanga upo, maji yapo kila kitu kipo, hivi wakifanya kazi usiku na mchana waseme mwezi wa nne wako tayari kukabidhi jengo shida ipo wapi...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amemtaka msimamizi wa ujenzi huo ambao ni Wakala wa Majengo Tanzani - TBA kuwasilisha katika ofisi yake taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo kwa kila mwezi hadi ujenzi huo utakapokamilika.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amesema Mkoa unaendelea na juhudi za kutunza mazingira hivyo kila shughuli itakayofanyika itazingatia utunzaji mazingira Mkoani humo.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania Mkoa wa Morogoro Mhandisi Rebeca Kimambo ambaye pia ni Mhandisi mshauri wa ujenzi huo amesema mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo mpya ya Mkuu wa Mkoa ulianza rasmi May 2022 na unatarajiwa kukamilika May 2024, ujenzi huo umefikia asilimia 50 na mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 2 sawa na asilimia 30 ya malipo yake.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.