Kufuatia mafuriko yaliyotokea Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro Disemba 5 mwaka huu na kuharibu miundombinu ya sekta mbalimbali ikiwemo maji, Barabara, Umeme, kilimo na Afya, Serikali Mkoani humo imedhamiria kuchukua hatua ya kudhibiti mafuriko hayo yanayotokea mara kwa mara Wilayani humo.
Hayo yamebainishwa Disemba 22, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa maagizo yake aliyokuwa ameyatoa kwa watendaji wa Serikali ngazi ya Mkoa kurudisha miundombinu iliyokuwa imeharibiwa na mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.
Mhe. Malima amesema kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara na kuharibu miundombinu, mali za wananchi wake na hata kusababisha vifo, hivyo amesema sio jambo jema kuendelea kulalamika kila yanapotokea mafuriko hayo na kutaka hatua za utafiti zaidi zifanyike ili kudhibiti mafuriko hayo.
“...hatuwezi tukawa tunalalamika sisi kila siku mafuriko...wenzetu wana utaratibu wa kuvuna maji kwa hiyo tuangalie namna ya kuyavuna haya maji yapate matumizi mengine kwa watu na hasa kwenye kilimo....” amesema Mkuu wa Mkoa Malima.
Mojawapo ya Mikakati ambayo ametaka ichukuliwe ni pamoja na kuvuna maji kwa kuchimba mabwawa ambayo yatakusanya maji yatakayotumika katika shughuli za kilimo kupitia umwagiliaji na shughuli nyingine za kibinadamu hususan kipindi cha kiangazi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ili kuondokana na kadhia hiyo kwa wananchi wa Kilosa ameagiza hatua za makusudi zichukuliwe kwa kuwaondoa wananchi wananoishi kwenye mabonde au mikondo ya maji na kuwapatia viwanja maeneo mengine ili kuepusha athari za uharibifu wa miundominu na mali zao.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza msukumo katika kurejesha miundominu iliyoharibiwa na mafuriko kupitia watendaji wake.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewashukuru Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Mhe. Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania – TANROADS kwa ushirikiano walioutoa katika kipindi chote cha mafuriko na kuhakikisha kuwa huduma za jamii zinarejea, pia amewashukuru Watendaji wa Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kutekeleza maagizo yake ya kurudisha huduma zilizokosekana wakati wa mafuriko hayo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha milioni 900 za kuboresha miundombinu Wilayani Kilosa ikiwemo kujenga mifereji ya maji na shilingi bilioni 69 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji ambacho kitazalisha lita 18000 kwa saa hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Mvumi na Vitongoji vyake.
Akitoa tathmini ya mafuriko hayo MKuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amesema kutokana na mafuriko hayo watu watatu wamepoteza maisha, Kaya 1470 zimeathirika, nyumba 316 zimebomoka na Ekari 303 za mashamba zimeathiriwa na maji. Ameongeza kuwa miundombinu ya barabara ikiwemo madajara matatu yalikatika huku akibainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 5.3 zinahitajika ili kuboresha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko.
Aidha, amesema hadi sasa mahitaji yanayohitajika ni pamoja na Vyandarua, Chakula, Magodoro, Dawa za kutibu maji, Sabuni, Mavazi, na vifaa vya shule kwa Watoto waliopoteza vifaa vyao.
Kwa upande wake Mhandisi Noel Mushi kwa niaba ya Meneja wa Bodi ya maji Bonde la WamiRuvu amesema utafiti uliofanyika kuhusu chanzo cha mafuriko hayo ni mvua zinazonyesha katika Mikoa ya Manyara katika Wilaya ya Kiteto na kwamba suluhisho pekee kwa sasa ni kujenga mabwawa manne yatakayopokea maji na kupunguza kasi ya maji hayo kutoka maeneo hayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.