Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa kijiji cha Lukinga Wilayani Gairo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amedhamiria kukuza uchumi wa wilaya ya Gairo kupitia Tarafa ya Nongwe ambayo amesema itakuwa kitovu cha mapinduzi katika sekta ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 15, 2023 wakati wa ziara yake ya siku moja katika Tarafa ya Nongwe Wilayani Gairo ziara iliyokuwa na lengo la kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kujionea maeneo ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara likiwemo zao la parachichi na karafuu.
Mazao mengine ambayo amesema yanastawi na kutaka yawekewe kipaumbele katika uzalishaji ni pamoja na kahawa, maharagwe, viazi mviringo na ndizi ambapo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo Bi. Sharifa Nabalang'anya na Afisa Kilimo wake kushauriana na kutoa elimu kwa wananchi ili kufikia lengo la kufanya mapinduzi ya kilimo katika Tarafa hiyo ya Nongwe kwa ajiri ya kuongeza kipato cha wananchi na kjongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Aidha, RC Malima amewaagiza Makatibu Tawala Wasaidizi sekta ya uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira na Sekta ya miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama kushirikiana na wananchi wa Tarafa hiyo kuweka mikakati na mipango madhubuti ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (wa tatu kushoto) akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Sharifa Nabalang'anya wakiangalia zao la kahawa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewashauri wakulima wa tarafa ya Nongwe kuacha kilimo cha mazoea ambacho hakina tija kwao badala yake amewaagiza wataalamu wa kilimo ngazi ya Mkoa na wilaya kutoa elimu ya kilimo cha kitaalam na kutenga mzeneo mahususi kwa ajiri ya uzalishaji wa mazao ya karafuu parachichi na kahawa.
Hata hivyo, katika sehemu ya miundombinu ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kukamilisha haraka kazi ya kuboresha barabara yenye urefu wa kilometa 62.5 ikiwa 55.5 km ili kurahisisha usafirishaji wa mazao hayo mara yatakapokuwa yahitaji kupelekwa katika masoko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuongea na wananchi wa kijiji cha Lukinga ambacho Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amekuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kufika tangu kisajiriwe mwa 1995 amesema serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuwafikia wananchi katika vijiji vyote bila kujali changamoto za barabara zilizopo huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa huo kuwa wa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kufika katika kijiji hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima akimuelekeza jambo Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe Jabir Makame wakati wakiangalia mazao mbalimbali yanayozalishwa Wilayani humo.
Nae, Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mhandisi Goefrey Mutakubwa akijibu swali la Mkuu wa Mkoa lililohusu uboreshaji wa barabara ya Nongwe, amesema bajeti ya barabara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 serikali imetenga Tsh. milioni 915 kwa ajili ya ukarabati wa umbali wa kilometa 55.5 ili wananchi wa tarafa hiyo kuwa na uhakika wa usafiri kwa kipindi chote cha mwaka.
Akiwa katika kijiji cha Lukinga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amewaunga mkono vijana 42 waliokwenda mkoani Njombe kupata mafunzo ya uzalishaji wa zao la Parachichi kwa lengo la kuja kuzalisha kijijini hapo, hivyo amewapa gunia Nne za mbegu ya parachichi kama alama ya kuwaunga mkono vijana hao.
Viazi mviringo ni miongoni mwa mazao yanayolimwa Wilayani Gairo.
Lakini pia amewaahidi kuwapa Tsh. 2,000 000/= ikiwa ni ghrama ya manunuzi ya mbegu walizootesha katika kitalu chao cha zao hilo na utaalamu huku pia akiahidi kukipa kikundi hicho cha vijana 42 fedha taslim 500,000 endapo wataazisha Akaunti ya benki kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha parachichi.
Hiki ni Kituo cha Afya Nongwe kilichopo Wilayani Gairo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.