Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoani humo kutoa elimu kwa wafanyabiashara itakayotoa matokeo chanya katika kuongeza ukusanyaji wa kodi Mkoani Morogoro.
Mhe. Adam ametoa agizo hilo Septemba 21, 2023 wakati wa kikao cha wadau wa sekta mbalimbali za uchumi wa Morogoro kilichofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kingsway Hotel uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kikiwa na lengo la kutatua changamoto za wadau hao katika kulipa kodi.
"... elimu iwe inclusive kwa ajili ya kuweza kuadress …..sasa niwaambie msiwazarau hawa waswahili wa mtaani ndio wanaoendesha uchumi wa nchi..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza viongozi hao kuangalia namna bora ya kukuza mitaji na uzalishaji kwa wafanyabiashara kwa kutoa elimu itakayowasaidia wafanyabiashara katika kukuza mitaji yao na sio elimu ya shule, kwani wafanyabiashara hao ndio chachu ya maendeleo katika Mkoa.
Sambamba na Hilo, Mhe. Malima amethibitisha kuwa Mkoa huo una fursa nyingi za uzalishaji mali ikiwemo mazao kama Kakao, Miwa na Karafuu, hivyo amezitaka taasisi hizo kutenga fedha kwa wazalishaji ili kuwa na walipa kodi wengi na wa uhakika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewataka wafanyabiashara kuifanyia kazi elimu inayotolewa kwao na TRA ikiwemo elimu ya matumizi mashine ya EFD kwani baadhi ya wafanyabiashara wameonekana hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na kufanya ukusanyaji wa mapato serikalini kuwa ya chini.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro Bw. Chacha Gotora amesema TRA itahakikisha inaboresha utoaji wa huduma na utengenezaji wa mahusiano kati ya ofisi yao na wadau mbalimbali wa kodi hususan kuwatembelea na kutambua changamoto mbalimbali walizo nazo zinazohusu kodi na kuzitatua.
Nae, Mwenyekiti TCCIA Mkoani humo Mwandhini Myanza amewaonya wafanyabiashara kuacha tabia ya udanganyifu kwa kutumia mfumo wa kielektroniki vibaya kwa kuwatolea wanunuaji wa bidhaa risiti zisizo na majina yao pamoja na gharama tofauti za manunuzi na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria huku akitoa angalizo kwa wafanya biashara hao kuwa makini katika kuangalia jina na gharama za risiti walizofanyia manunuzi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.