Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka waratibu wa chanjo na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwenye jamii Mkoani humo, kushirikisha wadau mbalimbali hususan viongozi wa dini kwenye zoezi la uhamasishaji wa chanjo ya Surua Lubera na utoaji dawa kwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama vile Usubi, Matende, Mabusha na Kichocho.
Mhe. Malima ameyasema hayo Februari 12, 2024 wakati wa kikao cha Afya ya Msingi kilicholenga uzinduzi wa kampeni ya Chanjo ya Surua Lubela na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Viongozi hao wa Dini wanaushawishi mkubwa kwenye jamii hivyo kupitia nyumba za ibada walizopo watahamasisha wananchi wengi kuitikia zoezi hilo la utoaji wa chanjo ya Surua na dawa za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambalo linatarajiwa kuanza Februari 15 hadi 18, 2024 Mkoani humo.
"...kwa sababu kwenye mambo haya ninyi hamuwezi kupeleka meseji kwa uwezo wanaopeleka... wao ijumaa, jumamosi na jumapili wanapata watu wengi kuliko utakaopata wewe..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amewataka wananchi kuacha kung'ang'ania mila, desturi na imani potofu hususan kwenye suala la chanjo kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amewataka waratibu hao kufikisha ujumbe kwa jamii kwa kutumia picha halisi ya madhara ya magonjwa hususan yale yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwenye jamii yakiwemo Matende, Mabusha, Usubi, Trakoma, Kichocho na Minyoo.
Naye, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembya amesema kampeni ya utoaji chanjo ya Surua Lubela Mkoani humo itafanyika ndani ya siku nne kuanzia Februari 15 hadi 18, 2024 na kuwafikia watoto 368555 wa Mkoa huo wenye umri kati ya miezi 9 hadi 59 huku akiwataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata chanjo hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Morogoro Dkt. Debora Kabudi amesema hapa nchini kuna magonjwa 5 ambayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele magonjwa hayo ni pamoja na Usubi, Kichocho, Matende, Minyoo ya tumbo na Mabusha.
Amesema, Mkoani Morogoro kuna ugonjwa wa Usubi ambao umeathiri Halmashauri 8 za Mkoa huo pia amebainisha kuwa Mkoa umeanzisha kampeni ya kutokomeza magonjwa hayo ikiwa ni pamoja na kutoa dawa za usubi, Minyoo ya tumbo na kichocho kwa wanafunzi wa shule za msingi ambapo zoezi linatarajiwa kuanza Februari 15, 2024.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.