Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amevitaka vyama vya ushirika vinavyojishughulisha na mifugo kufuga kisasa ili kuwa na mifugo bora itakayo kuwa na uzalishaji wenye tija kwao na taifa.
Mhe. Malima amesema hayo Mei 15, Mwaka huu wakati akifungua Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Morogoro lililofanyika ukumbi wa mikutano wa Mbaraka Mwinshehe uliopo Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Malima amesema faida ya kufuga kisasa na kuwa na mifugo bora kutaongeza pato la Serikali kwani wafugaji wataweza kulipa kodi kutokana na mifugo yao, kuendesha maisha yao hivyo kupunguza pia migogoro inayotajwa kuwa ni ya wakulima na wafugaji.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Maafisa Ushirika na Maafisa Mifugo wa Wilaya za Mvomero na Kilosa kuanzisha vyama vya Ushirika vya wafugaji na kuvipatia elimu ya kufuga mifugo yenye tija ili kuondokana na migogoro katika Wilaya zao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Adam Malima amewakumbusha wananchi wa Mkoa huo kwenda kuhakiki taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili itakayoanza Mei 16 hadi 22, 2025 ili kujipatia vigezo vya kupata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Naye, Mrajis Msaidizi wa uhamasishaji na uratibu TCDC Bw. Ibrahim Kadudu amesema vyama vya ushirika vinapaswa kuwekeza na kutoa fursa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ikiwa ni njia ya kusaidia kuimarisha jamii nzima.
Kwa upande wao wafugaji akiwemo Bi. Pendo Ndemo wa chama cha ushirika cha Namayana kutoka Mvomero wamekiri kuwa bado wanafuga bila kuzingatia utaalamu hali inayopelekea kupata faida kidogo inayotokana na mifugo hiyo hivyo wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia wataalam wa kutoa elimu kuhusu ufugaji wenye tija.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.