Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki kupima Afya zao wakati wa Kambi Maalum ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassani (Outreach Services) ili kukabiliana na magonjwa waliyonayo au yale ambayo wanayo bila ya wao kujua.
Mhe. Malima ametoa wito huo Aprili 29, Mwaka huu wakati akiongea na waandishi wa habari akitoa taarifa ya kambi hiyo itakayofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuanzia Mei 6 hadi 10 2024.
Mkuu wa Mkoa Adam Kighoma Malima amesema, kambi hiyo maalum inayojulikana kama ni ya kanda ya kati inayojumuisha Mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Pwani na wenyeji Morogoro itapokea wananchi wote wanaotaka kupata huduma hiyo maalum na yenye gharama nafuu kwa wananchi kutoka Mikoa hiyo iliyotajwa hapo juu.
Aidha, amesema, Kambi hiyo inakadiriwa kutoa huduma za afya kwa wagonjwa 200 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa 100 kwa siku watakazokuwepo kambini ambapo huduma zote za kumuona daktari zitatolewa kwa Tsh. 5000 pekee, hivyo wananchi wenye matatizo mbalimbali na wanaotaka kujua afya zao na kutaka ushauri watatakiwa kufika kambini hapo.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amewataka Wakuu wa Wilaya zote na Wakurugenzi kuhamasisha wananchi katika maeneo yao na kutafuta namna bora ya wagonjwa kuweza kujisajili na kufika katika kambi hiyo ili kupata huduma hiyo.
Hata hivyo amebainisha njia zitakazotumika katika kujisajiri mapema kabla ya siku au tarehe za kupata huduma hiyo ikiwemo wananchi kwenda kuwaona Wakuu wa Wilaya zao, kuwaona Wabunge wao na Wakurugenzi wa Halmashauri zao na hata kupiga simu ambazo ni 068343 5656 na 0783658931.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amesema kuwa Kambi hiyo itakuwa na Madaktari 54 ambao wanatoka katika Mikoa minne (4) ikiwa na lengo la kufikisha huduma kwa wananchi sambamba na kutoa ujuzi kwa madaktari waliokaribu na eneo la tukio, hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto nyingi za Afya kwa wananchi wa Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Singida na Dodoma.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dkt. Daniel Nkungu akijibu maswali ya waandishi wa habari alisema kuwa changamoto zote za kiafya zinazowakumba wagonjwa zikiwemo wanawake wanaosumbuliwa na uzazi, watoto, na kusisitiza kuwa WANANCHI WANAOHISI WAKO SAWA KIAFYA HUSUSANI WANAWAKE wafike kufanya vipimo vya afya (check up ) ili kupata ushauri na matibabu, kwan mara nyingi wznafika kufanya vipimo tayari wanakuwa wamechelewa na ugonjwa kuwa vigumu kutibika.
Katika kuhakikisha serikali inasogeza huduma za afya karibu na wananchi, Wizara ya afya kushirikiana na hospitali za rufaa za Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Singida na Pwani (Tumbi) itahusika kutoa huduma ya Afya kwa wananchi kupitia kambi maalum iliyoelezwa hapo juu.
Magonjwa yaliyopewa kipaumbele kutibu ni pamoja na magonjwa ya watoto, wanawake na uzazi, masikio, pua na koo, upumuaji, magonjwa ya ndani (Moyo, figo, kisukari na shinikizo la damu), mfumo wa mkojo, mifupa, ngozi, macho, kinywa na meno, Afya ya akili, utengamano, mfumo wa chakula na huduma ya usingizi tiba na ganzi.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.