Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ametekeleza ahadi yake aliyoitoa hivi karibu kwa Vijana wanaojitolea katika Jeshi la Zimamoto (Fire volunteers) waliounga mkono zoezi la uokoaji watu na mali zao baada ya kutokea mafuriko ya Januari 24, 2024 katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Malima amesema hayo Februari 5, 2024 wakati akikabidhi fedha taslimu kiasi cha shilingi 1,600,000/= kwa Vijana hao wa Fire Volunteers katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa mnamo Januari 24, mwaka huu yalitokea mafuriko maeneo mengi ya Mkoa huo ikiwemo maeneo ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu na mali za wananchi lakini Vikosi mbalimbali vilijitoa kusaidia zoezi la uokoaji.
Miongoni mwa vikosi hivyo ni pamoja na Fire Volunteers kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokaoji huku akibainisha kuwa alivutiwa kuona vijana hao wanajitoa kusaidia waathirika wamafuriko hayo na kuahidi kutoa milioni moja ili iwasaidie.
“...siku ile pale nikakuta kuna watu Volunteers maaskari wa Zimamoto na Uokozi wa kujitolea sasa lile jambo binafsi likanipa faraja kubwa sana...hnilisema mimi binafsi nitatoa milioni moja mkapate hata sababuni kwa wale watu 33 waliokuwepo pale...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itagharamia mafunzo ya muda mfupi ya ujuzi wa uokoaji yatakayopangwa siku za usoni ya Vijana hao huku Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani humo itahamasisha wadau wengine kuchangia vifaa wakati wa mafunzo ya vijana hao.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaasa vijana hao kuwa na nidhamu, maadili mema, utayari na kutambua kuwa jambo hilo ni la kujitolea hususan katika kipindi chote cha mafunzo.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Shabani Marugujo amesema lengo la kuanzisha Fire Volunteers ni kutokana uwezekano wa kutokea kwa majanga ya moto na mafuriko yanayosababishwa na kukua kwa teknolojia, ongezeko la watu na ukuaji wa miji, hivyo amesema Vijana hao ni muhim kuwa nao ili kuongeza nguvu katika zoezi la uokoaji.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Morogoro kwa sasa una vijana wa Fire Volunteers 74 huku akisema kuwa namba hiyo itaongezeka kutokana na mwamko wa Vijana kujiunga na kikundi hicho.
Kwa upande wake Kiongozi wa kikundi cha Fire Volunteers Mkoa wa Morogoro Salumu Selemani amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutimiza ahadi yake na kuongeza kuwa wameamua kuanzisha kikundi hicho kwa lengo la kuisaidia jamii wakati wa majanga.
Sambamba na shukrani hizo, Bw. Salum amewataka wananchi kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya majanga ambapo amewataka kupiga namba 114 kwa ajili ya kutoa taarifa mara wanapofikwa na majanga ya aina hiyo ili kupatiwa msaada.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.