Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea vikali tabia ya baaadhi ya watu kuwanyanyasa na kuwanyanyapaa wazee jambo ambalo ni kinyume na sheria na taratibu za nchi ambapo amesema jambo hilo hupelekea kudhohofisha maendeleo ya wazee.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Oktoba 1, 2024 wakati akizindua bwalo la wazee wa kituo cha Fungafunga pamoja na kusheherekea na kula chakula pamoja na wazee hao katika ukumbi wa kituo hicho kilichopo katika Halmashauri ya Manipsaa ya Morogoro.
Amesema, pindi wazee wanapotoka katika makazi yao na kupelekwa vituo vya kulelea wazee mali zao wanazoziacha katika makazi yao zitaendelea kuwa zao, hivyo amemtaka mwakilishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuliangalia suala hilo na kuweka sheria ya kuwalinda wazee kwa sababu imekuwa ni tabia ya baadhi ya watoto kuwapora mali wazee na kusababisha wazee kukosa haki zao.
".. Nikisema hili wanamorogoro wanisikie vizuri hii tabia ya kuwanyanyasa na kuwanyanyapaa wazee hiyo habari iishe kabisa kwa sababu hiyo ni akili ya watu wasiojielewa.." amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Malima amesema kituo hicho cha Fungafunga kinaweza kuhifadhi wazee 108 ambapo kwa sasa wapo wazee 23, hivyo amewataka wataalamu wa maendeleo ya Jamii kuliangalia suala hilo la kuwatafuta wazee wenye uhitaji katika Mkoa wa Morogoro na kuwapeleka eneo hilo kwa sababu nafasi bado ipo.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema suala la kuwapatia wazee huduma zao stahiki hasa huduma za Afya ni suala la lazima sio hiari, hivyo amewataka wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha suala la huduma kwa wazee linazingatiwa ili uhitaji wa huduma muhimu kwa wazee upapatikane kwa urahisi.
".. Hili suala la huduma kwa wazee litakuja kuwapa watu balaa tafuteni vitu vingine vya kufanyia masihara lakini sio jambo hili.." Amesisitiza kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kujali wazee kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya wazee na kuwakumbuka mara kwa mara hususan wakati wa sherehe mbalimbali.
Mwisho, Mhe. Malima amepokea changamoto zilizotolewa na wazee hao ikiwemo changamoto ya ubovu wa barabara inayoingia katika kituo hicho jambo ambalo amesema anaenda kulifanyia kazi na kuhakikisha barabara hiyo inapitika kipindi chote cha mwaka.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.