Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima ametembelea ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara inayojengwa kwa kiwango cha lami pamoja ujenzi wa Daraja la Ruaha na kuona utekelezaji wake huku akitoa maagizo kwa Mkandarasi anayejenga kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km 66.9 ifikapo mwezi Machi, 2024.
Mhe. Adam Kighoma Malima ametoa maagizo hayo Novemba 7 mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Wilaya za Kilombero na Ulanga na kufika eneo la mradi wa daraja hilo akiambatana na Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kutoa maagizo hayo huku ikataka viongozi wa Wilaya ya Kilombero kuendelea kushirikiana na Mkandarasi huyo ili akamilishe ujenzi huo kwa wakati.
"...matarajio yangu mimi ni kwamba muda huu tuliokubaliana basi hatutarajii kuona changamoto zingine hapo katikati, hapana..." amesema Mkuu nuyo wa Mkoa.
Akimsisitizia Mkandarasi huyo amesema, changamoto zozote zikiwemo mvua na nyingine zikiwapo anatakiwa kukabiliana nazo na kuongeza kasi ya ujenzi hususan wa Daraja hilo usiku na mchana kwa kuwa mradi huo ni wa muda mrefu na wananchi wanauhitaji ili kuonja matunda ya mradi huo.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amesema mradi huo ni kichocheo cha maendeleo katika ukanda wa bonde la Mto Kilombero kwa vile daraja na barabara hiyo ni kiunganishi pekee baina ya Wilaya zote za Ulanga, Malinyi na Kilombero lakini pia kiunganishi baina ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Songea ambapo kwa kukamilika kwake changamoto usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa hususan mazao itakuwa imetatuliwa lakini pia itakuwa ni rahisi kufika Mkoa wa songea kwa kupitia barabara hiyo.
Mradi mwingine uliotembelewa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Malima ni kituo cha kupoozea umeme kinachojengwa Mjini Ifakara ambacho ujenzi wake umefikia 99% na unatarajiwa kukamilika Mwezi Novemba 18, 2023 kwa gharama ya Tsh bil. 19.
Miradi hii yote inayoendelea kutekelezwa ndani ya Mkoa wa Morogoro ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa za miradi hiyo ya kimkakati na mingine mingi kwa ajiri ya wananchi wa Mkoa huo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.