Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa huo kuhakikisha wanafanya utambuzi wa wazee ndani ya Mkoa huo ili kuweza kufahamu idadi yao, kuwafikia na kuhakikisha wanapata huduma bora hususan huduma za Afya.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo Septemba 21, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee Duniani ambayo kimkoa yamefanyika Wilayani Gairo yakiambatana na kauli mbiu inayosema "Tuimarishe huduma kwa wazee, Wazeeke kwa Heshima".
Amesema, Mkoa wa Morogoro umefanya utambuzi wa wazee 56,000 ambapo wazee 51,000 kati yao wamepatiwa msamaha wa huduma mbalimbali, hivyo bado kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza jitihada ya kuwatambua ili kuhakikisha wanapata huduma zilizo bora na kwamba suala la wazee kupata huduma sio la hiari bali ni la lazima kwa sababu ni haki yao ya kimsingi.
"..Ninatoa maagizo kwa wakuu wa Wilaya na kwa Wakurugenzi, muende mkafanyie kazi suala la utambuzi wa wazee ili tuweze kuwafikia na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao.." amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Akibainisha zaidi, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa huo una jumla ya vikundi vya wazee wajasiliamali 25 ambapo vikundi 21 vipo Halmashauri ya Manispaa, Wilaya ya Kilosa 1, Mvomero 2, na Gairo 1 huku akiutaka uongozi wa wazee wa Morogoro kwenda kutoa elimu na kuhamasisha wazee kujiunga na vikundi vya ujasiliamali yakufanya biashara ndogondogo.
Aidha, Mhe. Malima amekemea vikali tabia ya baadhi ya vijana ya kuwapokonya wazee wao mali na kuzitumia jambo ambalo amesema ni kinyume na sheria na taratibu za nchi na kuwaagiza wazee ndani ya Mkoa huo kutofumbia macho masuala hayo na pindi matukio hayo yakitokea watoe taarifa haraka ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima ametumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Morogoro wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la kupiga kura na ifikapo Novemba 27, 2024 kwenda kupiga kura kwa sababu kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi ni haki ya kila mtanzania.
Akifafanua zaidi kiongozi huyo amebainisha kuwa Oktoba 11 hadi 20, 2024 kutakuwa na zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura huku akiwataka wazee kujitokeza kupiga kura lakini pia kuwahamasisha vijana kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura ili kupata viongozi bora wa kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa jumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Morogoro Bw. Samwel Mpeka ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo za kubaguliwa ndani ya jamii kwa sababu ya imani potofu, kutelekezwa na familia zao kutokana na ugumu wa maisha.
Changamoto nyingine ni pamoja na kutopata huduma za Afya na madawa, kwa sababu hiyo kupitia maadhimisho hayo ameiomba serikali kuendelea kuboresha huduma za Afya hasa utoaji wa dawa kwa wazee na kuendelea kutoa kadi za msamaha kwa wazee.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Wazee Mkoa wa Morogoro (MOROPEO) Bw. Samson Msemembo amesema kukomeshwa kwa ukatili wa mauaji ya wazee vikongwe, kudharauliwa na kunyanyapaliwa na kuimarisha hali ya maisha na ustawi itasaidi wazee wa nchi hii waishi kwa heshima.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.