Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kujiwekea utaratibu wa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kila kikao cha baraza lao ili kuiepusha uwepo wa utitiri wa hoja zinazopelekea kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa Adam Malima ametoa agizo hilo Juni 25 mwaka huu wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kilicho ukumbi wa FDC Ilonga Wilayani humo.
Maagizo hayo yamekuja baada ya Halmashauri hiyo kuwa na jumla ya hoja 27 zilizoibuliwa na CAG za tangu mwaka 2016/20217 na kupelekea kutotekelezwa kwa miradi ya maendeleo yenye jumla ya zaidi ya shilingi 1.8 Bil.
“nakuombeni sana ninyi madiwani, kila kikao chenu cha Baraza la madiwani muwe na ajenda za hoja za CAG” amesema Mhe. Malima.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri hiyo ya kilosa Kwenda kusimamia vema maendeleo ya wananchi wao ili wapate sifa zitakazowawezesha uchaguzi wa mwakani kurudi kwenye nafasi zao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoamwa Morogoro amewataka watendaji wote wa Mkoa huo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na kutoa onyo kwa watendaji watakaokwenda kinyume na miongozo hiyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha, amewataka Wahe. Madiwani pamoja na kuwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, bado amewataka Madiwani kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi ya maendeleo ikiwa ni alama ya nje ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitoa ushauri kwa madiwani na watendaji wa Serikali, Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Morogoro Bw. Baraka Mfugale amewataka kutoa ushirikiano wa kutosha wanapoomba nyaraka mbalimbali wakati wakitafuta majibu ya kufunga hoja, ili hoja hizo ziweze kufungwa mapema kabla hazijaingia kwenye vikao kama vinavyofanyika sasa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilibaki na hoja za miaka ya nyuma 2016/2017 hadi 2021/2022 ikiwa na jumla ya hoja 27 na mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya hoja mpya 12 ziliibuliwa.
Katika kutekeleza hoja hizo zilizoibuliwa na CAG, hoja 25 za nyuma kati ya hoja 27 zimekwishafungwa na kusaliwa na hoja mbili sawa na 92.59%. Aidha, hoja mpya 7 kati ya 12 zimefungwa na kusaliwa na hoja 5 sawa na 82%.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.