Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaomba wadau mbalimbali wa sekta za umma na binafsi kuendelea kutoa misaada yao ya hali na mali kwa lengo la kuwasaidia na kuwafariji waathirika wa mafuriko yaliyotokea takribani Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro.
Mhe. Malima ametoa wito huo Juni 28, 2024 wakati akipokea vifaa mbalimbali kutoka kwa Taasisi isiyo ya kiserikali ya The Islamic Foundation kwa ajili ya waathirika hao ikiwemo Nguo, Mafuta, Magodoro, Mashati na Madaftari kwa ajili ya wanafunzi pamoja taulo za kike.
"...tunawashukuru ndugu zetu hawa lakini tunatoa wito kwa ndugu zetu wengine kuiga mfano huu wa Islamic Foundation, bado Morogoro mahitaji ni makubwa..." Amesema Mhe. Malima
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema The Islamic Foundation wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa msaada wa Vifaa mbalimbali kwa waathirika na kubainisha kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii hususan ushirikiano waliouonesha wakati wa athari za mvua za El nino.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Adam Malima amewataka watendaji wote ngazi ya Halmashauri hadi kijiji kugawa misaada hiyo kwa utaratibu uliopangwa kulingana na tathmini itakayofanyika lengo ni msaada huo kuwafikia walengwa na si vinginevyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa The Islamic Foundation Sheikh. Arafat Badru amesema wamepeleka msaada huo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa sababu wameona kuwa hapo ndipo mahali sahihi na salama kwa msaada wao kuwafikia walengwa na kwamba msaada huo una thamani ya takrabani shilingi 30 Mil.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.