Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wakazi wa Mkoa huo na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya miaka 80 ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro tangu kuanzishwa kwake na kuwataka wakazi hao kushiriki matembezi ya hisani kwa ajili ya maboresho ya Hospitali hiyo.
Ametoa wito huo Mei 13, 2025 wakati anaongea na waandishi wa habari kuelezea tukio la maadhimisho ya miaka 80 ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Morogoro yatakayofanyika Mei 17, 2025 yakiwa na kaulimbiu inayosema "MIAKA 80 YA UJENZI WA JAMII YENYE AFYA ".
Mhe. Malima amesema, lengo la maadhimisho hayo ni kuakisi huduma za Afya za hospitali hiyo zilizoanza kutolewa tangu mwaka 1945 na kuonesha maendeleo makubwa kwa miaka hiyo 80 na hivyo kuona umuhim wa kuadhimisha mafanikio ya Hospitali hiyo kwa kufanya matembezi ya hisani ili kuboresha baadhi ya miundombinu ya Hospitali hiyo.
"...nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushiriki kikamilifu katika maadhimishohayo na matembezi ya hisani." Amesisitiza Mhe. Adam Malima
Aidha, kiongozi huyo amesema maadhimisho hayo yalianza na programu ya upimaji wa Afya kwa wananchi tangu Mei 5 hadi Mei 9 mwaka huu ambapo jumla ya wananchi 3,772 wamepatiwa huduma za vipimo (Afya Check) na kufanyiwa huduma za upasuaji wagonjwa 170 bure hususan wagonjwa walioshindwa kupata huduma hizo kwa sababu za kukosa fedha na kwamba huduma za upasuaji zinaendelea kutolewa hadi tarehe 16 Mei, 2025 ili kukamilisha upasuaji kwa wagonjwa 242 waliokusudiwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa fedha nyingi kwa kipindi kifupi cha miaka yake minne ya uongozi Wake katika sekta ya Afya ambapo Hospitali hiyo imepokea zaidi ya shilingi billioni 7.8 kwa ajili ya kuboresha hudumaza Afya Pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za dharura.
Amebainisha pia kuwa fedha hizo zimesaidia kujenga majengo ya huduma za dharura, jengo la wagonjwa mahututi, uwekaji vifaa vya kisasa vya kutolea huduma kama CT Scan, Digital X-Ray, Mtambo wa kufua hewa tiba ya oksjeni, Kifaa cha uchunguzi wa sikio, koo, pua, mashine kumi za kuchuja damu (Dialysis) na uboreshaji wa huduma za Daraja la kwanza.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro inatimiza miaka 80 tangu ilipoazishwa mwaka 1945 ikiwa kama kituo cha kutolea huduma za Afya kwa majeruhi wa vita ya pili ya Dunia iliyoanza mwaka 1939 - 1945.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.