Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, ametoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro kushiriki Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yatakayoanza kufanyika kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 8, 2025.
Mhe. Malima ametoa wito huo leo Julai, 29, 2025 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake na kubainisha kuwa maonesho hayo yanaenda sambamba na kaulimbiu inayosema;
“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025.”
“Nitoe wito kwa wananchi wa mikoa hii minne, hususan wenyeji wa Mkoa wa Morogoro, kufika kwa wingi katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius K. Nyerere na kushiriki kikamilifu katika maonesho haya,” amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Amesema, maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika kwa asilimia 98, huku maboresho mbalimbali yakiendelea. Moja ya maboresho hayo ni upatikanaji wa maji changamoto ambayo imekuwa sugu kwa wadau wa maonesho hayo.
Aidha, ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali yake kwa kutoa fedha zilizotumika kuchimba visima vya maji na kusambaza kwa wananchi na eneo la Viwanja vya Maonesho ya Nanenane.
Mhe. Malima amewataka viongozi wa Serikali mkoani humo kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi wakati wote wa maonesho hayo, huku akiwahakikishia washiriki ulinzi wa kutosha ndani ya viwanja vya nanenane kanda ya Mashariki na Mkoa mzima kwa jumla.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amesema Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yatahusisha jukwaa maalum la B2B (Business to Business), litakalotumika kutoa mada zinazohusu Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na mazao yatokanayo na misitu zitakazowasilishwa na wakufunzi wabobezi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
Amesema, mada hizo zitatolewa bila malipo kuanzia Agosti 2 hadi hadi Agosti 7 na kwa sababu hiyo amewataka wananchi wote wenye nafasi kushiriki jukwaa hilo ili kupata maarifa na ujunzi katika masuala ya kilimo, Mifugo, Uvuvi na masuala na misitu.
Mgeni rasmi wa maonesho hayo ya Nanenane kanda ya Mashariki mwaka 2025 yanayotarajiwa kuanza Agosti 1 na kufunguliwa rasmi Agosti 2 ni Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la taifa la Uashauri wa Rais wa masuala ya Kilimo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.