Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amekemea vikali baadhi ya wananchi wasio wema kuhamasisha wananchi kutokujiandikisha kwenye orodha ya daftari la mpiga kura wa Serikali za Mitaa ili kupata fursa ya kuchagua viongozi bora wenye kuleta maendeleo ya Jamii.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa tamko hilo Oktoba 16, Mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lupiro Wilayani Ulanga kwa lengo la uhamasishaji wa uandikishaji wa wananchi kwenye orodha ya mpiga kura wa Serikali za Mitaa ulioanza Oktoba 11 hadi 20 Mwaka huu ili kuweza kushiriki Uchaguzi.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amewasisitiza wananchi hao kuachana na baadhi ya watu wanaopotosha kutokushiriki katika zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Aidha, Mhe. Adam amesema Wilaya za Malinyi na Ulanga kumekuwa na muitikio hafifu kwenye uandikishaji kwani Wilaya hizo hazijafikia asilimia 40 kwa kulinganisha na takwimu ya Oktoba 16 ya nchi nzima ambayo ni asilimia 47 ya uandikishaji wananchi kwenye orodha ya mpiga kura wa Serikali za Mitaa.
"... maeneo mawili Ulanga, Malinyi mpaka hivi tunavyozungumza ninyi uandikishaji wenu upo chini ya asilimia 40 asitokee mtu kupotosha wenzie wasijiandikishe..." Amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Kwa sababu hiyo, Mhe. Malima amewasisitiza wananchi wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye kujiandikisha ili kupata haki ya msingi ya kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwani zimebaki siku nne pekee za kufanikisha zoezi hilo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amesema wazazi na walezi wanajukumu la kuhakikisha wanatoa malezi yaliyo bora kwa watoto ili waweze kutimiza ndoto zao na kuwataka kuendeleza utekelezaji wa kampeni "tuwaambie kabla hawajaharibikiwa" inatarajiwa kuwafikia vijana wa ngazi zote za elimu hapa nchini.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amekemea migogoro ya wakulima na wafugaji inayosababishwa na wafugaji kulisha mazao ya wakulima katika Wilaya hiyo hususan kwenye kijiji cha lukande na kudokeza kuwa wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuleta maendeleo katika jamii pasina migogoro yoyote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ulanga Bi. Saida Mahugu amesema Wilaya hiyo imepanga kuandikisha wananchi zaidi ya 130,000 lakini hadi kufikia Oktoba 15 Mwaka huu umefikia asilimia 40 hivyo wameendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha ili kuwa na haki ya kupiga kura.
Naye, Diwani wa kata ya Lukande Mhe. Novatus Majid amesema kata hiyo inawakazi zaidi ya 9000 na 4000 pekee ndio wenye vigezo vya kujiandikisha, kati ya wananchi hao waliojiandikisha ni 1500 hiyo imetokana na baadhi ya wananchi kukaa mbali na vituo vya kujiandikishia hivyo wameweka mpango mkakati wa kuwafikia huko walipo ili wananchi wote wapate nafasi ya kujiandikisha.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.