Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaonya Maafisa Manunuzi Mkoani humo wenye tabia ya kuchelewesha taratibu za manunuzi kwa maslahi yao kuacha tabia hiyo mara moja badala yake kuharakisha taratibu hizo ili kuleta ufanisi wa shughuli za Serikali ikiwemo kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
Mhe. Malima ametoa onyo hilo Februari Mosi, 2024 wakati wa kikao cha mapitio ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ikiwa ni muendelezo wa vikao vya mapitio ya bajeti za Halmashauri za Mkoa huo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa miradi ya maendeleo mingi Mkoani humo imekuwa ni viporo moja ya sababu ni ucheleweshwaji wa manunuzi ambao baadhi yake una walakini kwa maslahi ya mtu binafsi jambo ambalo amelikemea vikali.
“...yani mtu anakuambia hatujafata taratibu sijui nini huyo ni muongo na dili la kupiga halija kamilika...watu wa kwanza kukanyaga ni hawa maafisa manunuzi...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Akitolea mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amesema kuna miradi mingi haijakamilika na muda wa ukamilishaji wa miradi hiyo umepita lakini miradi bado iko hatua za awali za manunuzi.
Hivyo, amewataka kuhakikisha kuwa taratibu za manunuzi zinafanyika kwa wakati hususan kwenye miradi ya Afya, Elimu na Maji na kwamba hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya maafisa watakaobainika kujihusisha na uzembe huo.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.