Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaonya baadhi ya wafugaji wenye tabia ya kulishia mifugo yao mazao ya wakulima kwa makusudi na kwamba tabia hiyo ikome mara moja badala yake waheshimiane.
Adam Kighoma Malima ametoa agizo hilo Juni 10, 2024 wakati wa ziara yake akiambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kufanya ziara ya kukagua miundombinu mbalimbali Mkoani humo itakayofanyika kwa siku tatu.
Akiwa katika Kitongoji cha Mtakenini Wilayani Mvomero kukagua matengenezo ya Barabara ya Doma – Kilosa - Maharaka alipokea kero kutoka kwa wananchi wa kitongoji hicho namna wanavyosumbuliwa na baadhi ya wafugaji kulisha mifugo kwenye mazao yao likiwemo zao la nyanya.
Mhe. Adam Malima amesema, ni vema makundi hayo mawili ya Wafugaji na wakulima yakaheshimiana kwa kuwa kila upande umehiari wenyewe kufanya kazi wanayoifanya, hivyo mkulima amheshimu mfugaji na mfugaji amheshimu mkulima kwani kila mmoja kachagua kazi hiyo kwa hiari yake.
Hata hivyo, amekemea vikali baadhi ya wafugaji wanaoingiza mifugo yao kwa makusudi kwenye mashamba ya wakulima na mifugo yao kula mazao ya wakulima na kwamba huo ni udhalimu wa kiwango cha juu na kuitaka tabia hiyo ikome mara moja.
“nakwambia Mkuu wa Wilaya na wewe Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri tengenezeni utaratibu ili Mvomero tabia hii ife kabisa na ikome” amesisitiza Mhe. Malima
Amewataka wafugaji kama wanataka kulisha mazao ya wakulima wafanye utaratibu wa kuingia makubaliano na wenye mazao kwa kulipa fedha ili mkulima apate haki yake na mfugaji aweze kulisha mazao hayo kwa uhuru zaidi
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewageukia Watathmini Mali wanaokadiria hasara inayotokana na mifugo kula mazao ya wakulima kuacha tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wafugaji na kukadiria hasara hizo chini ya kiwango kinachotarajiwa.
Naye Meneja wa Maji Mijini na Vijijini – RUWASA amemwahidi Mkuu wa Mkoa wa Morogorokukamilisha mradi wa maji unaoendelea kukamilishwa katika eneo hilo mwishoni mwa mwezi huu wa Juni huku Mkuu wa Mkoa akiongeza wiki mbili hivyo Julai 15 kaqzi ya kuwapelekea wananchi hao maji iwe imekamilika.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakenini kwa niaba ya wananchi wenzake kero sugu zinazowasumbua katika eneo lao ni Pamoja na Barabara, Wanyama tembo kuvamia mashamba yao pamoja na uhaba wa maji.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.