Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewashukuru wananchi wa kata ya Lundi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa kuitikia fikra ya maendeleo kwa kuanza kupanda miche ya michikichi pamoja na kuandaa vitalu vya miche hiyo kwa ajili ya kuongeza kipato cha Halmashauri, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Malima ameyasema hayo Januari 10, 2024 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi Mkoani humo.
Mhe. Malima amesema miche elfu 60 ambayo wanakijiji wa Kata ya Lundi wameletewa imetoka katika kitalu cha Serikali ambapo imegawanywa kwa Wananchi hao ili kuzalisha miche mingine kupitia miche waliyoletewa kwa ajili ya kuongeza idadi ya miche ili kila mwanakijiji aweze kupata miche kwa ajili ya kupanda.
“...nawashukuru wanalundi kwa kuitikia hii fikra, ambayo ni fikra ya maendeleo na kwa maana hii ninyi mmehamasisha na sisi tunakwenda kufungua milango ya kuhakikisha tunakwenda kuwapata watanzania wengi zaidi...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kwa kutoa miche ya michikichi 100,000 kwa ajili ya kuwagawia Wanamorogoro hasa wa Kata ya Lundi.
Hata hivyo, Mhe. Malima amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Florence Mwambene kuuboresha mradi wa kamua mafuta ya mawese uliopo Kata ya Lundi na kuufanya kuwa rasmi na kuweka mazingira mazuri ya sehemu ya uzalishaji unayoendelea.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lundi Mhe. Ally Hussein Mkata amesema wananchi wa Kata hiyo wamehamasika kwa kuanza kutayarisha mashamba yao kwa ajili ya kupanda miche ya michikichi, pia ameahidi kutoa shamba kubwa kwa ajili ya shughuli ya upandaji wa miche hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.