Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wahe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kusimamia miradi ya maendeleo kikamilifu kwa kuwa Halmashauri hiyo ni moja ya majukumu yao ya Msingi katika kuhakikisha wanawapelekea wananchi maendeleo na kukuza kipato chao.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Juni 29, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo Mkoani Morogoro.
Kiongozi huyo amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa wahe. Madiwani wa Halmashauri hiyo kusimamia miradi ya maendeleo inayopelekwa na Serikali kwa wananchi, hivyo wanatakiwa kuwajibika katika kuisimamia miradi hiyo na endapo watashindwa kuisimamia watakuwa wameshindwa kufanya kazi yao ya msingi.
“.. Kazi yenu madiwani ni kusimamia miradi ya maendeleo, madiwwni wasiosimamia ni sawa na mtu anayeulizwa swali kuhusu kwake halafu hajui…” amesema Adam Malima.
Kiongozi huyo amebainisha ndani ya kikao hicho, kazi nyingine za msingi za Wahe. Madiwani ukiachia usimamizi wa miradi ya maendeleo ni pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za Serikali na kusimamia Halmashauri zao katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri zao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima ameagiza watumishi wa Halmashauri hiyo ambao hawajahamia makao Makuu ya Halmashauri hiyo, kuhamia mara moja kabla au ifikapo Agosti 1, mwaka huu na ambaye hatatekeleza agizo hilo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, ameelekeza kuwa watendaji wote ambao wanakabiliwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha au mali za Umma ambao wametajwa kwenye Hoja za CAG, watumishi hao watafutwe na jeshi la polisi, wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ama mamlaka zinazohusika.
Akisisitiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wahe. Madiwani kutumia mfumo huo katika kuuza mazao ya wakulima wa Halmashauri hiyo kwa kuwa unamlinda mkulima kutonyonywa na una maslahi mapana kwa Halmashauri yao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kufanya kazi zao kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo, akisisitiza masuala mengi ikiwemo utunzaji wa siri za Ofisi, kutojihusisha na rushwa, usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo na uwasilishaji wa fedha Benki za makusanyo ya ndani ya halmashauri.
Kwa upande mwingine amewashauri Wahe. Madiwani pamoja na kutekeleza miradi iliyoletwa na Serikali na kutekeleza kilimo cha mazao ya kimkakati kikiwemo kilimo cha zao la michikichiki, parachichi, Kokoa, Chai na mazao ya viungo kama Karafuu bado kuna fursa nyingi za kuzitumia katika kukuza uchumi wa wananchi wao ikiwemo matumizi sahihi ya mashina ya migomba ambayo huzalisha nyuzi za kutengenezea vifaa mbalimbali vinavyotumika na jamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Lucas Lemomo wakati akiahirisha kikao hicho kwa niaba ya Wahe. Madiwani wengine ametumia fursa hiyo kupongeza uongozi wa Mkoa namna ulivyosaidia kuongeza nguvu katika kusimamia ujenzi wa shule za sekondari ikiwemo shule ya Mkoa wa Morogoro na pia amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kutekeleza maelekezo yote ya ufungaji wa hoja za CAG kama kikao hicho kilivyoelekeza.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.