Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wahe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kusimamia miradi ya maendeleo kikamilifu ili kuweka msukumo wa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa manufaa ya wananchi.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Juni 22, 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro.
Kiongozi huyo amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wahe. madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kusimamia miradi ya maendeleo inayopelekwa kwa wananchi na kuwajibika kuisimamia na pindi watakaposhindwa kuisimamia miradi hiyo watakuwa wameshindwa kufanya kazi yao ya msingi.
".. Kazi yenu nyie madiwani ni kusimamia miradi mkishindwa kusimamia mtakuwa mmeshindwa kufanya kazi yenu ya msingi.." amesisitiza Adam Malima.
Aidha Mhe. Malima amewasisitiza watumishi wa Wilaya hiyo kufanya kazi kwa maslahi mapana ya wanaulanga na sio kwa maslahi yao binafsi, pia watumishi kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano baina yao kwa lengo la kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema hataki kusikia wahe. madiwani wanaingia kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji bali wao waende kusimamia haki kwa watu wanao onewa na baadhi ya wafugaji ili kupunguza migogoro hiyo baina ya wakulima na wafugaji.
".. sitaki kusikia kabisa kuwa wahe. Madiwani ni sehemu ya migogoro ya wakulima na wafugaji bali nendeni mkatoe haki kwa watu wanao onewa.. " amesisitiza Adam Malima.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.