Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Ali Kighoma Malima amewataka viongozi wa dini kuwa mfano katika kupambana na mmomonyoko wa maadili hapa nchini na kuwafundisha vijana kudumisha maadili na tamaduni za kiafrika ili kuwa na kizazi kitakachokuwa na tija katika maendeleo.
Mhe. Malima amesema hayo Novemba 19, 2023 alipohudhuria Baraza la maulidi la Mkoa wa Morogoro lililofanyika kata ya Dakawa Wilayani Mvomero Mkoani humo ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema maadili ya jamii yetu yanaharibiwa na utamaduni wa mataifa ya Maghaharibi kupitia mitandao ya kijamii hususan vijana ambao ndio tegemeo kwani wameanza kubadili jinsia ya kiume kutaka kuwa jinsia ya kike, ya kike kuwa ya kiume na matumizi ya dawa za kulevya sambamba na mienendo isiyofaa ambayo hukwamisha juhudi za serikali za kufikia malengo iliyojiwekea.
"...kwa hiyo niwasihi ndugu zangu tunatakiwa kuwa mfano katika kupambana na madawa ya kulevya kwa kushirikiana na Serikali ili kulinda kizazi hiki na kijacho..." amesema Mhe. Adam Malima
Katika hatua nyingine, Mhe. Adam Malima amesisitiza Baraza hilo kuhakikisha kuwa na Masheikh waliosoma Elimu ya dini ya kiislam na kuijua vizuri katika kuendeleza vema elimu hiyo kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Morogoro Sheikh Twaha kilango amethibitisha kutoa ushirikiano katika uongozi wake na serikali ili kupunguza baadhi ya majukumu ikiwemo kutoa elimu ya kimaadili kwa wananchi ili kuinusuru jamii ya kitanzania kuathirika na tamaduni zisizofaa.
Naye, Amili wa ujenzi wa misikiti sehemu zisizo na misikiti Mkoani Morogoro Sheikh Ibrahim Musa Makange amesema mmomonyoko wa maadili ikiwemo utumiaji wa madawa umekithiri hususan kwa vijana ambao ndio tegemeo la Taifa, hivyo amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuendelea kuchukua hatua ili kuleta maendeleo ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.