Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi wa Wilaya ya Gairo na Mkoa kwa ujumla kufanya mapinduzi ya Sekta ya Kilimo hususan Kilimo biashara kutekeleza kwa vitendo ili kuongeza thamani katika Sekta hiyo na kuwa mfano kwa Watanzania wote.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 12, 2024 wakati akifunga maonesho ya SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024, MSIMU WA 3 yaliyofanyika Wilayani Gairo kuanzia Oktoba 6 - 12, Mwaka huu yakiwa na lengo la kuwasaidia wakulima na wafugaji kupata huduma na kujifunza teknolojia mpya na mbinu bora za uzalishaji.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema maonesho hayo yamefanyika kwa msimu wa tatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo hivyo amewataka wananchi hao kuchangamkia fursa katika sekta ya Kilimo kama wanavyo himizwa ili kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo, kuongeza mapato, kuboresha maisha na kujipatia kipato kwa uzalishaji wa wenye maslahi mapana ya nchi.
"..Ombi langu mimi hii jitihada kubwa inayofanywa ili wananchi wa Gairo wanufaike na mapinduzi ya Kilimo nakuombeni msiwe watu wa kusikiliza bila kufanyia kazi, muwe mnayafanyia kazi na watanzania wengi watakuja kuiga kutoka kwenu.." Amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Pia Mhe. Malima amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kulima mazao ya kimkakati yakiwemo Tumbaku, mbaazi, parachichi ili kuondokana na umasikini kwani kilimo Wilayani humo ni muhimili wa vipato vya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewaagiza wataalamu wa kilimo kuendelea kushirikiana na wakulima na wafugaji ili kupata uelewa kuhusu matumizi ya pembejeo za kilimo, mbegu, mbolea na sumu za kuua wadudu kwa uzalishaji wenye tija na kuongeza mapato katika Halmashauri hiyo na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Adam amehimiza wananchi wa Wilaya hiyo kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni kuunga mkono ajenda ya Mhe. Dkt. Samiaa Suluhu Hassan kwa maono ya kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo Gesi, umeme, mkaa mweupe na nyingine ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yakiwemo magonjwa ya kansa ya mapafu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira akiongea kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa huo Dkt. Mussa Ali Mussa amesema zaidi ya asilimia 65% ya wananchi wa Mkoa huo wanategemea kilimo hivyo amewataka wananchi hao kufanya kilimo chenye tija.
Kwa sababu hiyo, Kiongozi huyo ametoa wito kwa viongozi mbali mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Tarafa, Katibu Tawala wa Wilaya, Watendaji wa Kata, Maafisa kilimo na Maafisa Ugani waliopo ngazi ya Kata na vijiji kuhakikisha elimu za kilimo bora zinawafikia wananchi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.