Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka Watumishi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuiletea halmashauri hiyo maendeleo kwa faida ya wananchi wake.
Mhe. Adam Malima ametoa kauli hiyo Januari 31, 2024 wakati wa kikao cha kupitia na kuhakiki bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni muendelezo wa Vikao vya kupitia na kuhakiki bajeti za Halmashauri zote za Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ili Halmashauri iweze kupata maendeleo ni muhim kwa watendaji wake kuwa wamoja, kushikamana na kufanya kazi kama timu huku akiwasisitiza kuachana na mitafaruku isiyo na tija kwenye utendaji wao.
“...nyie nendeni amueni kufanya kazi kama timu mchukueni huyo bibi (Mkurugenzi) semeni ni boss wenu fanyeni kazi mtafanya maajabu hapa...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, kwenye kikao hicho Mhe. Malima amewataka watendaji kusimamia suala nzima la ukusanyaji mapato na kuwa na matumizi sahihi ya mapato hayo na kuwataka kubuni vyanzo vya mapato vingine kuliko kutegemea fedha zinazotokana na mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Nao wajumbe wa kikao hicho akiwemo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa ameitaka Halmashauri hiyo kutenga fedha kwa mwaka 2024/2024 kwa ajili ya kununua madawati, viti na meza kwa shule za msingi ambazo zimekosa madawati miundombinu hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji hao kukamilisha miradi yote viporo ambayo muda wake wa ujenzi umeshapita lakini miradi hiyo haijakamilika na kuitaka ikamilike kabla au ifikapo mwezi Machi mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.