Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amezindua rasmi ujenzi wa stendi ya mabasi ambayo itaunganishwa na Kituo cha Reli ya Mwendokasi cha Jakaya Mrisho Kikwete cha mjini Morogoro, ujenzi utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.4 Mradi unatarajiwa kukamilika Julai 21, 2026.
Mhe. Malima amefanya uzinduzi huo Julai 23, 2025 huku akiwataka wafanyabiashara wa Mkoa huo kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwekeza katika eneo hilo ili kulifanya liwe la kisasa na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amezitaka taasisi zinazoshughulikia maji, umeme, barabara na Halmashauri yenyewe kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kabla ya kukamilika kwa ujenzi huo ili stendi hiyo iweze kuwa bora na ya kisasa hivyo kutoa huduma za kiwango cha juu kwa wananchi.
Mhe. Malima ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo, akisema kuwa ni ishara ya dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha wananchi wa Morogoro wanapata huduma bora na kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Emmanuel Mkongo, amesema ujenzi huo utahusisha majengo mbalimbali, likiwemo jengo la ghorofa moja litakalojumuisha hoteli yenye vyumba 30 vya kulala wageni, eneo la vinywaji na burudani, ukumbi mkubwa wa mikutano na ndogo nne na maduka.
Maeneo mengine ya jengo hilo ni mabanda ya kisasa kwa ajili ya mama lishe na baba lishe, kituo cha polisi, maeneo ya kupaki mabasi, bodaboda na bajaji, pamoja na sehemu za kukaa abiria na kubainisha kuwa ujenzi huo utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria kutoka kituo hicho kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Manispaa.
Naye Ramadhani Juma Mfinanga mwananchi wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni dereva wa bajaji, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mradi huo, kwani amesema utaongeza idadi ya abiria, jambo litakalowaongezea kipato na kuboresha maisha yao.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.