Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amezipongeza timu za Simba na Yanga kwa kuingia hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku akibainisha kuwa jambo hilo limeipa heshima nchi na kuitangazaTanzania kwa kuingiza timu mbili katika hatua hiyo.
Mhe. Malima ametoa pongezi hizo Machi 6, 2024 wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa timu ya Simba SC akiwemo Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Bw. Imani Kajula ambao walifika ofisini kwa Mkuu huyo wa Mkoa kumtembelea.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Tanzania kupeleka timu mbili kwenye hatua ya robo fainali kwenye mashindano hayo ni kutokana na uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya michezo hapa nchini pamoja na uongozi imara wa nchi na timu hizo.
“...mimi kama mdau wa mpira wa miguu naomba niwapongeze sana na niwashukuru mmetuheshimisha...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima akisisitiza suala la michezo kwa jumla amesema, kuna haja ya kukuza vipaji vya ndani ya nchi ili kwa siku za baadaye nchi iwe na wachezaji wengi wa ndani na wengine wapate nafasi ya kucheza timu za nje.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Mkoa utafanya kila jitihada katika kuendelea kuboresha uwanja wa Jamhuri ili uweze kufanana na uwanja wa Benjamini Mkapa na kuwaomba viongozi wa timu hizo kumshika mkono ili jambo hilo lifanikiwe.
Naye, Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba SC Bw. Imani Kajula kwa niaba ya Uongozi na wachezaji wa timu hiyo, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maandalizi na mapokezi ya timu hiyo na kuongeza kuwa timu ya Simba itatumia uwanja wa Jamhuri kama uwanja wa nyumbani kwa michezo mitano wakianza na mchezo wao dhidi ya timu ya Tanzania Prisons utakao chezwa katika uwanja wa Jamhuri Machi 6, 2024.
Bw. Imani Kajula amemuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa watamsaidia kufanikisha dhamira yake ya kuboresha uwanja huku akiweka bayana kuwa timu yao ina wachezaji wengi wa timu B vijana kutoka mkoani Morogoro ambao baadae watakuwa tishio na kuahidi kurudi tena mkoani humu rasmi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zinazofanyika katika kukuza vipaji.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.