Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani humo kumkamata mwenyekiti wa Kijiji cha wami luhindo Wilayani Mvomero, Juma Makumlo kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za wananchi wa kijiji hicho.
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa agizo hilo Septemba 2 mwaka huu akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani Mvomero wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Wami Luhindo.
Shigela amemtaka Mwenyekiti huyo anayetuhumiwa kukamatwa mara moja na kurejesha fedha zote alizokuwa anazipata kutoka kwa wananchi wake kwa kuwachangisha michango isiyo halali na kisha kutokomea na fedha hizo kusikojulikana.
“Nataka leo mtafute mwenyekiti, mkamate na kesho aitoe hiyo laki moja irudi kwenye kijiji” ameagiza Martine Shigela.
Kutokana na kadhia hiyo, Martine Shigela ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Mvomero kufuata utaratibu wote wa kiutumishi na kukasimisha shughuli za mwenyekiti wa kijiji hicho kwa Mwl. David Langa ambaye atafanya kazi za kupokea michango kutoka kwa wananchi na kusimamia shughuli nyingine za kijiji hicho.
Aidha, Shigela ameuagiza uongozi huo kumsainisha mkataba Mwl. David Langa kabla ya kuanza majukumu hayo mapya huku akiwaagiza pia kuanza kumlipa mshahara wake kwa muda wote atakaokuwa anakaimu nafasi hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wa Kijiji hicho kutokuwa na hofu yoyote kila mara viongozi wa Serikali wanapopanga kutembelea Kijijini kwao kwani hawana nia mbaya badala yake wana lengo la kutaka kuwaletea kutatua nkero zao na kuwaletea maendeleo yao
“msitishike, mimi nimekuja kutatua kero na matatizo ya wanakijiji, kama walikuwepo viongozi wenu wa vijiji wakawajengea hofu mimi nimekuja kwa ajili ya wananchi” amesema martine shigela.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mvomero Halima Okash amesema amepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa aliyoyatoa na amemhakikishia kuyatekeleza na kufuatilia kwa karibu agizo la kutiwa nguvuni Mwenyekiti anayetuhumiwa kukimbia na fedha za wananchi.
Kwa upande wao Wananchi wa kijiji cha Wami Luhindo wamemueleza Mkuu wa Mkoa matatizo yao, akiwemo Bw. Marick Abdallah ambaye amesema mojawapo ya matatizo ya kijiji hicho ni suala zima la ujenzi wa madarasa kusimama tangu mwaka 2014, pamoja na uhaba wa madawati unaopelekea watoto wao kukaa chini.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa Martine Shigela amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mvomero ikiwemo bwawa la umwagiliaji mtwiba sugar, ujenzi wa shule ya sekondari ya kumbukumbu ya hayati Moringe Sokoine pamoja na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Manyinga kilichopo katika tarafa ya Turiani.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.