Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuagiza meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kukarabati na kuchonga barabara inayotoka Mgeta hadi Ifakara Mji ili kurahisisha Mawasiliano Wilayani Kilombero.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo Juni 13, 2024 wakati wa ziara yake pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Mkoa huo ya kukagua miundombinu mbalimbali.
"... tulichokubaliana ni nini, kutoka hapa Mgeta hadi Ifakara ni km 77 kwa wananchi wanaweza kutumia siku nzima, sasa nimemwambia huyo bwana achonge hii barabara kwa namna yoyote wakati tukisubiri lami..." amesema Mhe. Malima
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesikitishwa na hali ya barabara hiyo iliyoharibiwa na mafuriko ya mvua za El-nino na kutaka TANROADS kuwa wabunifu kwa kuchonga barabara hiyo ili kupitika vizuri na kuruhusu maji kupita katika mitaro wakati wananchi wakisubiri barabara ya kiwango cha lami.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amewataka wakandarasi wanaopewa tenda hizo kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa muda uliopangwa kwa lengo la kusaidia wananchi ambao ndio wenye uhitaji mkubwa wa miundombinu kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Mhe. Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha za dharura kwa ajili ya ukarabati miundombinu ikiwemo madaraja na barabara za Mkoani humo kutokana na athari za mafuriko ya Mvua za El-nino.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba kwa kushihirikiana na TARURA kuangalia namna watakavyowafidia wakazi wenye nyumba zao ambazo ziko karibu mno barabara ya kuingia Makao makuu ya Halmashauri hiyo kwa kuwa nyumba hizo ziko hatarini na sio salama kwa kuishi eneo hilo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.