Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ameahidi kufanya mashindano makubwa Mkoani Morogoro ili kuendeleza vipaji vya watoto na vijana kwani madrasa huongeza maarifa,utii, juhudi, heshima na maadili mema ya kufanya vizuri kwenye masomo ya madrasa na shuleni pia.
Amesema hayo Machi 16 Mwaka huu wakati wa Mashindano ya Qur-an yaliyoandaliwa na Umoja wa Waalim wa Madrasa wa Morogoro (UWAMAMO) yaliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Bomaroad uliopo Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Mwassa ametatua changamoto ya vifaa kama printer itakayotumika kwa ajili ya kuchapa nakala mbalimbali ikiwemo mitihani.
“ kama nitakuwepo Mkoa wa Morogoro mwakani mwezi kama huu wa Ramadhani natarajia nishirikiane na Kamati hii kuafanya mashindano makubwa hapa Mkoani Morogoro”…. Amesema Mhe. Fatma Mwassa
Aidha, Mhe. Mwassa amewaomba wanamorogoro kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi yatakayofanyika kitaifa Mkoani Morogoro ambapo Mgeni rasmi atakuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAMAMO Alhaji Sheikh Mohamed Salim Masenga amesema lengo la Mashindano hayo ni kuhifadhi Qur-an kwa watoto na vijana ili kuepuka tabia zisizofaa kwani madrasa hufundisha vijana kuwa na nidhamu, hekima, na busara katika kupambanua mambo ya kidunia na kuilinda Qur-an isipotee.
Nae Katibu wa UWAMAMO Bw. Haafidhi Hussen Mbanachi amesema Mashindano hayo huinua uwezo na ufahamu kwa watoto na vijana katika maisha ya dini ya kiislamu na ametoa wito kwa wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao watokapo madrasa.
Mjumbe na Mlezi wa UWAMAMO Bw. Bachoo Sidik Bachoo amesema mashindano hayo huondoa mabaya yaliyopo katika jamii kwani Qur-an huongoza kwa misingi na taratibu zilizopo na ni sehemu ya kulinda vijana kuingia katika mambo yasiyofaa kama ulevi, rushwa, madawa ya kulevya, na ushoga ili kuwa na idadi kamili ya nguvu kazi hapa nchini.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.