Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema atatumia Askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) waliopo Mkoani humo kusaidia kulinda vyanzo vya maji, hifadhi za misitu na mazingira kwa ujumla ili kuhakikisha Morogoro ya zamani inarudi katika hali yake ya awali.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa kauli hiyo Novemba 4, mwaka huu wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya jeshi hilo la akiba kundi la 22/22 katika viwanja vya Fulwe, Tarafa ya Mikese Wilaya ya Morogoro.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya jeshi la akiba yeye ndiye kamanda wa jeshi hilo kimkoa, hivyo niwakati mwafaka mwake kutumia jeshi hilo kulinda vyanzo vya maji ili kupunguza makali ya mgao wa maji na kupata umeme wa uhakika hususan umeme unaotokana na maji.
“...lakini leo nimekuja kuwaambia kwamba nyie kwa sasa sio akiba, nawahitaji sasa sio badae... nikiwa kamanda wa jeshi la akiba naanza kutumia vikosi vyangu vya jeshi la akiba...” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Aidha, amesema kwa sasa Serikali ina kazi ya kulinda vyanzo vya maji, Ina kazi ya kuzuia uchomaji wa moto milimani pamoja na kulinda mipaka ya hifadhi za milima ili kuzuia wavamizi wanaojenga makazi yao katika maeneo hayo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza siku Saba kwa jeshi hilo la akiba kuendelea kujifunza mbinu za kuzima na kuzuia moto matukio ambayo yamekuwa sugu Katika Mkoa huo.
Hata hivyo ameagiza Mshauri wa jeshi hilo la akiba Mkoa wa Morogoro kuanzia mwakani jeshi hilo lianze kupewa masomo ya ujasiliamali kwa kipindi chote Cha mafunzo yao ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi Mara wanapohitimu mufunzo yao.
Sambamba na agizo Hilo amemtaka Mshauri huyo kuratibu mafunzo ya mgambo Kufanyika Tarafa zenye vyanzo vya maji ili kuongeza ulinzi wa maeneo hayo ambayo ni muhim kwa Mkoa na taifa kwa jumla.
Akitoa tathmini ya idadi ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa mwaka huu, Mshauri wa Jeshi la akiba Mkoa wa Morogoro Kanali Valentine Makyao amesema Wilaya ya Morogoro ndiyo imeongoza kuwa na idadi kubwa ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa Mkoa huo kwa kuwa na wahitinu 160, ukilinganisha na Wilaya nyingine za mkoa huo.
Aidha, Kanali Makyao amesema uwepo wa jeshi hilo la akiba linaongeza uwezo wa kuimarisha Ulinzi na Usalama Katika maeneo mbalimbali hapa nchini huku akitumia fursa hiyo kumuomba mgeni rasmi kusaidia vijana hao kupata mashamba ili wajiajiri kupitia kilimo kwa kuwa Mkoa huo ni mkoa wa Kilimo hivyo wakiwezeshwa kupitia fedha za asilimia 10, zinazotolewa na Halmashauri wanaweza kujikita kwenye Kilimo cha mazao ya kimkakati kama vile mazao ya karafuu na mkonge.
Kwaniaba ya wahitimu wa mafunzo hayo Bw. Nassoro Ally, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi wahitimu hao wamemuomba mgeni rasmi kupewa kipaumbele kwenye ajira pindi zinapotokea hususan zile zinazohusiana na mafunzo waliyoyapata ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto sugu ya ajira.
Mafunzo hayo ya mgambo ambayo yalianza Julai 4 mwaka huu yakiwa na wanafunzi 174, kati yao 14 hawakuweza kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, utovu wa nidhamu na kuugua.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.